NA MWANDISHI WETU, MWANZA
MSIMU wa Tatu wa Kampeni ya kuhamasisha utamaduni wa Kuweka Akiba na Benki ya NMB ‘NMB Bonge la Mpango’, umezinduliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Paulo Chacha, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima, ambako zawadi zenye thamani ya Sh. Mil. 180 – zikiwemo pesa taslimu, bodaboda, pikipiki za mizigo za matairi matatu na vifaa vya nyumbani vya kieleltroniki, zitatolewa katika kipindi cha wiki 12.
Bonge la Mpango msimu huu itafanyika kwa miezi mitatu kuanzia leo Jumatano Machi 29, chini ya kaulimbiu ya ‘Moto Uleule – #Hatupoi’, ikilenga sio tu kuhamasisha uwekaji akiba, bali pia kurejesha kwa jamii sehemu ya faida yake, huku pia ukiwa ni mkakati wa NMB kuendelea kuwa chaguo la kwanza la wateja kwa usalama wa fedha zao pamoja na uhakika wa huduma bora na rafiki za kibenki nchini.
Uzinduzi wa Bonge la Mpango – Moto Uleule imezinduliwa kwenye Soko la Buhongwa wilayani Nyamagana jijini Mwanza, ambapo DC Chacha aliishukuru NMB kwa kuuchagua mkoa wake kuwa sehemu ya kuzindulia kampeni hiyo, huku akiipongeza kwa kutenga zawadi kubwa na nono kwa ajili ya kuwazawadia wateja ambao wanaweka akiba kwa manufaa yao wenyewe.
Katika hafla hiyo ya uzinduzi wa NMB Bonge la Mpango, madereva 10 wa bodaboda, bajaji na matoroli wanaoendesha shughuli zao katika Soko la Buhongwa, walifunguliwa akaunti na RC Malima, DC Chacha na Mameneja Waandamizi wa NMB na kuwekewa kiasi cha Sh. 100,000 kwa kila mmoja ili kukidhi kigezo kikuu cha kuingia kwenye droo promosheni hiyo na kushinda zawadi.
“Kampeni hii ikawe chachu ya kujenga utamaduni chanya wa kujiwekea akiba, ambalo ni jambo zuri na muhimu katika maisha, ambayo yana dharura na changamoto nyingi sana zinazohitaji fedha katika utatuzi wake, na kama hauna unapata wakati mgumu zaidi, lakini kwa mwenye akiba haitomsumbua sana.
“Tunaweka akiba kwa manufaa yetu, lakini NMB wao wanaamua kutuzawadia fedha na vifaa mbalimbali, zikiwemo bodaboda na pikipiki za miguu mitatu ambazo ni mtaji mzuri kibiashara, ambao mimi mwenyewe natamani kushinda na kwa mantiki hiyo nitatumia vema akaunti yangu wakati huu na nikipata pikipiki ya tairi tatu itanisaidia Sana,” alisisitiza DC Chacha.
Aidha, Chacha alienda mbali zaidi na kuishukuru NMB kwa namna inavyojitoa kusaidia sekta za elimu na afya, huku akifafanua kuwa shuleni na mahospitalini mkoani Mwanza kumetapakaa uwezeshwaji wa benki hiyo, aliyoitaka kujipongeza pindi itakaposikia kiwango cha ufaulu kimepanda mkoani mwake, kwani ni kitakuwa kimetokana na mchango yao.
Awali, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, licha ya kurejesha faida kwa jamii na kuchagiza tabia ya uwekaji akiba miongoni mwa wateja, wataitumia kampeni hiyo kuwapa elimu ya umuhimu wa kutotumia tu akaunti zao kwa ajili ya kupitishia fedha, bali kuzitumia kuwekea akiba zao kwa manufaa yao ya baadaye.
“Bonge la Mpango limekuwa jambo kubwa mno kwa sasa, lililochangia kuongezeka kwa wanaoweka akiba katika akaunti zao. Ni kampeni itakayotoa zawadi mbalimbali kila wiki, kila mwezi na fainali itakayofanyika mwishoni mwa promosheni hii miezi mitatu ijayo.
“Jumla kuu ya thamani ya zawadi mbalimbali za ‘Bonge la Mpango – Moto Uleule’ ni Sh. Mil. 180 zitakazoshindaniwa na wateja wetu wote wenye akiba inayoanzia Sh. 100,000 ama wateja wapya watakaofungua akaunti nasi wakati huu na kuweka akiba inayoanzia kiwango hicho na kuendelea,” alisema Mponzi mbele ya Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Baraka Ladislaus.
Mponzi alibainisha kuwa katika kipindi hicho washindi 90 watajishindia pesa taslimu Sh. 100,000 kila mmoja (washindi 10 kila wiki – sawa na Sh. Mil. 9) na washindi wawili kila wiki wakishinda Sh. 200,000 kila mmoja. Katika kila wiki (kwa Wiki tisa) NMB itakabidhi bodaboda moja moja yenye thamani ya Sh. Mil. 2.5 ambapo zote 9 zitakuwa na thamani ya Sh. Mil. 22.7.
Zawadi nyingine ni kwa wateja 10 wa droo za kila mwezi ambao watashinda bodaboda zenye thamani ya Sh. Mil. 25, huku wateja wengine 10 wa kila mwezi wakitarajiwa kujishindia pesa taslimu Sh. Mil. 1 kila mmoja (sawa na Sh. Mil. 10 kwa wote).
“Katika ‘Grand Finale,’ NMB itatoa pikipiki tano za miguu mitatu ‘Toyo’, thamani ya kila moja ni zaidi ya Sh. Mil. 5.5 (zote Sh. Mil. 25.55), lakini pia itakuwa fainali ambayo wateja wetu wengine watano watajinyakulia friji la milango miwili, TV, ‘smartphone,’ ‘washing machine’ na kompyuta mpakato ‘laptop,’ vyote vikiwa na thamani ya Sh. Mil. 14.1,” alibainisha Mponzi.