*DK. MPANGO ATOA MATUMAINI YA RAIS DK SAMIA KUPANDA KWA MISHAHARA, MABORESHO ZAIDI YANAENDELEA, ASIHI UMOJA NA MSHIKAMANO KWA WAFANYAKAZI
Na MWANDISHI WETU
-ARUSHA
NI mwanga mpya. Ndivyo unaweza kusema hasa baada ya Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutangaza matumaini ya kupada kwa nyongeza ya mishahara kama wafanyakazi walioomba.
Kauli hiyo ya matumaini imetolewa jana Jijini Arusha na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, alipokuwa akihutubia katika kilele cha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani, Mei mosi kwa niaba ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Kutokana na hali hiyo, Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango amewaondoa hofu wafanyakazi nchini kuhusu ongezeko la mishahara na kuwapa tumaini kuwa hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan atasema jambo.
Alisema licha ya changamoto zinazoikumba dunia na kuathiri mifumo mbalimbali, Taifa linajivunia uchumi stahimilivu.
“Tathimini ya Serikali na taasisi za kimataifa zimeonesha kuwa uchumi wa Taifa umekuwa stahimilifu kwa kiwango cha kuridhisha, hivyo Mama wa Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan amenituma niwaambie wafanyakazi kama mambo yakiendelea hivi atasema jambo hivi karibuni,” alisema Dk. Mpango.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Mpango alitoa wito kwa wafanyakazi nchini kuendelea kuchapa kazi kwa maslahi ya Taifa kwa kutanguliza uzalendo.
MISHAHARA KWA WATUMISHI 473
Hata hivyo msaidizi huyo namba moja wa Rais Samia, alieleza uamuzi wa Serikali kuamua kulipa mishahara ya Watumishi 473 kutoka Halmashauri 101 kutokana na hamshauri hizo kushindwa kulipa mishahara hiyo kupitia mapato ya ndani.
Dk. Mpango alisema zaidi ya Shilingi billion 3.5 zimetengwa kuzipiga jeki halmashauri hizo.
“Kuanzia mwezi Julai 2024, jumla ya Wafanyakazi 473 kutoka Halmshauri 101, watalipwa kupitia Mfuko Mkuu Serikali ambao ni zaidi ya Shilingi bilioni 3.5,” alisema Dk Mpango.
Pamoja na hali huyo, Dk. Mapngo amezitaka halmashauri zote nchini kubuni vyanzo vya mapato ili kuipunguzia mzigo Serikali.
LIKIZO YA UZAZI
Hata hivyo, Dk. Mpango amewataka waajiri wote nchini kuwapa muda zaidi wa likizo wafanyakazi wanaojifungua watoto njiti ili kuhakikisha ustawi wa afya ya mama na mtoto.
“Mfanyakazi atakapojifungua mtoto njiti, kipindi cha uangalizi hakitahesabiwa kuwa sehemu ya likizo yake ya uzazi,” alisema kiongozi huyo
Aidha, alisema mzazi anapaswa kutoka kazini Saa 7:30 Mchana kila siku kwa muda wa miezi sita baada ya kujifungua ili apate muda zaidi wa kunyonyesha.
Katika hatua nyingine, Dk. Mpango amewataka wafanyakazi nchini kusimama katika weledi na kuacha uzembe wawapo kazini.
“Kwa Wafanyakazi ambao hawatumii nafasi zao ipasavyo watumie siku hii kujitafakari,” alisema na kuwaasa wafanyakazi hao