Na MWANDISHI WETU
-MOROGORO
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amevunja ukimya akieleza sababu iliyomfanya atumbuliwe katika nafasi ya Uwaziri mwaka 2017.
Machi 23, 2017, Rais wa Aamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli alimtumbua Nnauye katika nafasi ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Dk. Magufuli alimteua Dk. Harrison Mwakyembe kuziba nafasi ya Nnauye aliyemtumbua na kuapishwa Machi 24,2017 Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Nnauye alitumbuliwa katika nafasi hiyo siku moja baada ya kupokea ripoti ya kamati ya uchunguzi aliyuoiunda kuhusu uvamizi.
Uvamizi huo ulifanywa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwenye Studio za Kituo cha Clouds, jijini humo.
Katika ripoti yao, kamati hiyo ilimkosoa Makonda ikisema alitumia vibaya mamlaka yake na kupendekeza Nnauye awasilishe malalamiko ya waandishi wa habari dhidi ya Makoda kwa Hayati Magufuli.
Pia kamati ilipendekeza kuanzishwa uchunguzi dhidi ya polisi waliongia na Makonda katika kituo hicho cha utangazaji wakiwa na silaha za moto.
Nnauye aliwataka viongozi wa umma kufanya kazi kwa weledi, kuahidi kuikabidhi ripoti hiyo kwa mamlaka za juu zaidi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kutokana na mapendekezo yaliyomo.
Kabla Nnauye hajaiwasilisha ripoti hiyo kwa mamlaka, Hayati Dk. Magufuli alimtumbua katika nafasi hiyo.
Wakati akifungua Mkutano wa 12 wa kitaaluma wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ambao unaendelea mkoani Morogoro, Nnauye alisema kufukuzwa kwake Uwaziri kulimpa heshima kibwa.
Alisema hakujutia kufukuzwa kazi kwa kutekeleza wajibu wake kama kiongozi aliyekuwa na dhamana ya kufuatilia sakala hilo bali alichozingatia, kukisimamia ni kulenda heshma yake ya kusimamia haki.
Alisema kabla ya kupokea ripoti hiyo, alipata taarifa za kuachana na jambo hilo ili asipoteze kazi kwa kufuatilia tukio lakini alisimamia msimamo wake wa kuhakikisha hatua stahiki zinachokuliwa juu ya tukio hilo jambo ambalo halikumfurahisha mwenye mamlaka.
Katika hatua nyingine, TEF ilitoa tuzo rasmi kwa Nnanye ikitambua mchango wake mkubwa kwenye tasnia ya habari hata kusababisha apoteze Uwaziri mwaka 2017.
Pia TEF ilitoa tuzo kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro kwa kutambua mchango wake uliofanikisha kuanzishwa jukwaa hilo.