Na MWANDISHI WETU
-DODOMA
TUME ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC) chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia, inaendelea na utekelezaji wa hatua za awali za upembuzi yakinifu wa mabwawa sita ya umwagiliaji kwaajili ya kunusuru mradi wa reli ya kisasa (SGR).
Mabwawa hayo yanajengwa katika maeneo ya Kidete mkoani Morogoro na Kimagai, Dabalo, Hombolo, Ikowa na Buigiri yaliyopo mkoani Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa, akiwa ameongozana na wataalamu kutoka Shirika la Reli nchini,wataalamu wa Tume pamoja na wataalamu wa Benki ya Dunia na wale wa Bonde la Wami Ruvu wakati wa kufanya ziara ya matayarisho ya kuanza kazi ya upembuzi yakinifu amesisitiza umuhimu wa mradi huo kwa kuwa mabwawa hayo yataimarisha usalama wa mradi wa SGR.
Mndolwa alisema timu hiyo ya wataalamu wametembelea mradi wa bwawa la Kidete mkoani Morogoro na bwawa la Membe, Msagali, Kimagai, Hombolo na Dabalo mkoani Dodoma, kwa lengo la kujionea hali halisi ya mabwawa hayo
“Utekelezaji wa miradi hiyo ya mabwawa unalenga kuvuna maji ya mvua ili kuzuia mafuriko kwenye reli ya kati sambamba na kuendeleza kilimo cha umwagiliaji mkoani Morogoro na Dodoma,” alisema
Mradi huo wa kukabiliana na mafuriko, unahusisha ujenzi wa mabwawa mapya pamoja na ukarabati wa mabwawa yaliyokuwepo awali ambayo ni bwawa la Hombolo na Dabalo.
Katika hatua nyingine wataalamu wa Tume ya Taifa ya Uwagiliaji (NIRC) wamewezeshwa kupata mafunzo juu ya usalama na matayarisho ya ujenzi wa mabwawa hayo ikiwa ni miongoni mwa hatua za awali katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi na ukarabati wa mabwawa hayo.
Lengo ni kuhakikisha ujenzi huo unafanyika kwa ufanisi na kuwezesha kuvuna maji,kuzuia mafuriko na kulinda reli ya kati katika mikoa ya Dodoma na Morogoro.
Mafunzo hayo yametolewa jijini Dodoma na wataalamu kutoka Benki ya Dunia kwa lengo la kuwakumbusha wataalamu wa Tume kuzingatia usalama wa mabwawa katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi, ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea ikiwemo vifo na uharibifu wa makazi na miundombinu mingine.
Katika mafunzo hayo wataalamu hao wamepatiwa elimu ya kutambua viashiria vya hatari kwa upande wa mabwawa pamoja na namna bora ya kujiandaa ili kupunguza au kukabilina na madhara yanayoweza kutokea ikiwa mabwawa yatakoyojengwa na yanayoendelea kujengwa, yataonesha dalili zozote za hatari.
Vilevile, wataalamu hao wamekumbushwa kuhusu sera na sheria za mabwawa; kutoka kwa wataalamu wa Wizara ya Maji, ikiwemo umuhimu wa kuzingatia lengo la serikali la kujenga uwezo wa usalama wa mabwawa utakaosaidia miundombinu hiyo kudumu kwa muda mrefu zaidi.
Benki ya Dunia imedhamiria kuunga mkono kwa dhati ujenzi wa SGR nchini Tanzania, ambapo mradi huo wa reli unaolenga kubadilisha miundombinu ya usafiri unakwenda kufungua njia ya usafiri wa kisasa wa reli ya umeme, kuunganisha mikoa muhimu ndani ya nchi na nchi jirani. Ili kulinda SGR kutokana na mafuriko.
Benki ya Dunia inashirikiana na TRC, NIRC, na Wizara ya Maji ambapo Wadau hawa kwa Pamoja, wamejidhatiti kushikirikiana katika ujenzi wa mabwawa ya kukusanya maji ya mvua, kwa namna itakayo imarisha usalama wa SGR; pamoja na kuwezesha upatikanaji wa maji yatakayo tumika kwa matumizi ya binadamu, wanyama, uvuvi pamoja na kilimo cha umwagiliaji