Home KITAIFA NMB YATOA MIKOPO YA TRILIONI 1.7/- SEKTA YA KILIMO MIAKA MITANO

NMB YATOA MIKOPO YA TRILIONI 1.7/- SEKTA YA KILIMO MIAKA MITANO

Google search engine
Mkuu wa Mtandao wa Matawi ya Benki ya NMB, Donatus Richard akiwahudumia baadhi ya wateja waliyotembelea Banda la NMB kwenye Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Tanzania yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam leo. Na Mpigapicha Wetu

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

BENKI ya NMB imefichua siri ya mwamko wa Wadau wa Sekta ya Kilimo kuchangamkia Mikopo ya Kilimo-Biashara, ambako ndani ya miaka mitano imekopesha zaidi ya Shilingi  Trilioni 1.7 na kuiwezesha sekta hiyo kupiga hatua na kuongeza tija kwa wakulima wadogo, wa kati na wakubwa.

Sekta ya Kilimo inayotajwa kuchangia asilimia 30 ya Pato la Taifa na kuajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania, ni mnyororo wa thamani unaojumuisha kilimo chenyewe, uvuvi na ufugaji, ambako NMB inakopesha na kuwawezesha wadau wake, kwa kushirikiana na taasisi washirika, ikiwemo Kampuni ya Agricom Tanzania.

Akizungumza kwenye Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Tanzania, yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Meneja Mwandamizi wa Idara ya Kilimo-Biashara wa NMB, Neema Melleyeck, ametaja siri ya mwitikio huo kuwa riba nafuu, elimu, ushauri na masuluhisho ya kifedha wanayotoa.

Alisema, NMB kwa kutambua umuhimu wa Sekta ya Kilimo kwa Uchumi wa Tanzania, ilishusha riba ya mikopo ya kilimo hadi kufikia ‘single digit’ asilimia 9, pamoja na kusaini makubaliano na Agricom kuhakikisha wakulima wanakopeshwa matrekta, ‘power tiller,’ zana nyingine za kilimo na pembejeo.

“Lengo kuu ni kuiwezesha Sekta ya Kilimo kupiga hatua nchini, lakini pia kuongeza tija kwa wakulima, wadogo, wa kati, wakubwa na wadau wote wa mnyororo huo wa thamani unaojumuisha pia wavuvi na wafugaji, ambao licha ya kukopeshwa, hupewa elimu na ushauri juu ya mikopo yao kwa ufanisi wao kiuchumi.

“Hii imetufanya NMB kuwa benki tunayoongoza kunufaisha wadau wa sekta hii, ambapo tayari tumeshatoa mikopo ya zaidi ya Shilingi Trilioni 1.7 ndani ya miaka mitano hadi mwaka jana, wanufaika wakiwa wakulima wa kada zote na wafanyabiasaha zinazofungamana na kilimo.

“Mwamko mkubwa wa Watanzania kukopa umetokana na NMB kushusha riba hadi kufikia asilimia 9, tukijielekeza zaidi katika mikopo ya Stakabadhi Ghalani, Kilimo cha Mkataba na Mikopo ya Uwekezaji kwenye kilimo na Kuongeza Uzalishaji wa mazao,” alisema Neema.

Alifafanua ya kwamba, mikopo ya benki katika Sekta ya Kilimo inaanzia pale mkulima anapochagua ardhi, anapolima, anapopanda mbegu, kupalilia, kuvuna, kupeleka masokoni na kuwaunganisha wakulima na wadau wengine wakiwemo wateja wa mazao yao.

“Mkulima anaweza kukopa zana za kilimo kwa kulipa asilimia 20, kisha benki inamdhamini asilimia 80 na jambo jema ni ukweli kwamba NMB sio tu mikopo, bali elimu sahihi inayozunguka sekta yenyewe, riba nafuu na huduma zenye masuluhishi ya kifedha,” alisisitiza.

Katika kuhakikisha mchango wa Sekta ya Kilimo kwa Uchumi wa taifa unaongezeka, Juni 27 mwaka jana 2023, NMB ilisaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) na Kampuni ya Agricom Tanzania, yaliyolenga kukuza na kuleta mabadiliko chanya katika kilimo.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here