*ASEMA ALIYEFUNDISHWA DINI HAWEZI KUFANYA HIVYO, AWASHANGAA WANASIASA WANAOENDELEA KUTUSI, KUDHALILISHA
Na MWANDISHI WETU
-ZANZIBAR
RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa dini zote nchini kukaa na kufundisha vijana kufuata mafundisho ya dini huku akisema kuwa watu waliopitishwa kwenye mafunzo ya dini hawawezi kusimama wakanyanyua midomo kuwatusi au kuwakashifu viongozi wao.
Kauli hiyo aliitoa leo Julai 5, 2024 Jijini Zanzibar katika Kongamano la Wanawake wa Kiislamu, alisema anashangazwa na tabia iliyojengeka kwa baadhi ya watu wakiwamo wanasiasa kuwatusi viongozi.
“Wakati mwingine nikisoma kwenye mitandao ya kijamii, nikisikiliza hotuba za wanasiasa wenzetu jinsi wanavyowachambua na kuwadhalilisha viongozi wetu napata mashaka kama kweli tumepata malezi ya kiimani au kwetu dini hii tunaifanya kama utamaduni tu au mila bila kufuata na kuwa na imani ya kweli na dini yetu.
“Nimekuwa nikisema mara kadhaa kwamba watu waliopitishwa kwenye mafunzo ya dini hawezi kusimama akanyanyua mdomo akamtusi au akamkashifu kiongozi wake hawezi, kwa hiyo wale wanaofanya ni kwa sababu hawakupita kwenye malezi ya kidini na wito wangu huwa nasema na viongozi wa dini zote kukaa na kufundisha vijana wetu.
“…majukwaa ya siasa yana hamasa, yana ashiki, yanashawishi mtu akikaa kwenye jukwaa basi yanamtoka tu, tuongeze jitihada kwa vijana wetu, kwa watu wetu tuwe na milimi laini,” alisema Rais Samia
KIONGOZI NI KIVULI
Aidha Mkuu huyo wa nchi, alisema kuwa kiongozi anatakiwa kuwa mti wa kivuli ambapo wananchi wenye shida na uhitaji wanamwendea na kupata utatuzi wa masuala yao.
Pamoja na hali hiyo alissisitiza umuhimu wa wananchi kuwaheshimu viongozi wao katika ngazi zote, pamoja na kueleza wajibu na sifa za viongozi wanaotakiwa.
Rais Samia, alisema kuwa ni muhimu wananchi kuheshimu viongozi wao, sio tu wa kisiasa, hata wa dini, hata kama wanatoka kwenye kundi dogo ndani ya jamii kwani Mungu aliona kitu ndani yao ndiyo sababu akawapa dhamana ya uongozi.
“Na sisi viongozi tunao wajibu wa kuendelea kuishi katika misingi ya uongozi bora, tunatakiwa kuwa waadilifu, tuwe sadiki na tuwe weledi,” alisema na kusisitiza kuwa kiongozi anatakiwa kuwa na kauli moja atakayoisimamia, sio leo anasema hiki, kesho anabadili na kusema kingine. Alisema viongozi wakiwa na sifa hizo, wananchi na wanaowafuata watawaheshimu na kuendelea kuwaamini