Na MWANDISHI WETU
-PWANI
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanzisha rasmi kampeni maalumu ya kliniki za ardhi zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini iliyopewa jina la Samia Ardhi Kliniki.
Kauli hiyo imetolewa wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa Wakati wa ufunguzi wa kliniki ya ardhi ya wilaya hiyo ambayo itasikiliza na kutatua migogoro ya ardhi ya wananchi.
Waziri Silaa ameziagiza ofisi zote za ardhi nchini kutoa huduma kwa uwazi na sio kutoa huduma kwa kujifungia, ili wananchi waweze kusikilizwa pasipo kificho.
Aidha, amesema wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imefikia uamuzi wa kuanzisha mikoa miwili ya ardhi katika Mkoa wa Pwani, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan ambapo mikoa hiyo ni
Pwani Kaskazini wenye Halmashauri ya Kibaha, Chalinze na Bagamoyo na Pwani Kusini wenye Halmashauri za Mkuranga, Kisarawe, Mafia na Kibiti.