Na MWANDISHI WETU
-IRINGA
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM) Mohammed Ali Kawaida , amewasihi viongozi wa UVCCM mikoa na wilaya zote nchini, kujifunza namna ya kuishi kwenye misingi ya uongozi kwa vitendo huku wakizingatia Katiba, Kanuni na miongozo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Pia amewataka viongozi hao, kuhamasisha ushiriki wa vijana kikamilifu katika uandikishaji katika Daftari la kudumu la Wapiga kura linazotazamiwa kuzinduliwa rasmi Julai 20, mwaka huu mkoani Kigoma.
Kawaida ameyasema hayo alipokua anahutubia viongozi na watendaji hao katika ufungaji wa mafunzo ya viongozi na watendaji wa UVCCM mikoa na wilaya zote nchini yaliyofanyika Chuo chua Ihemi mkoani Iringa kuanzia Julai 11 hadi 17, 2024.
Alisema mafunzo hayo waliyoyapata yanastahili hivyo yataenda kurahisisha utendaji kazi wao katika maeneo yao ya kazi.
“Niwasihi sana nendeni mkaishi katika misingi ya uongozi kwa kuzingatia Katiba, Kanuni na miongozo ya chama chetu.
“Nimefurahishwa sana namna ambavyo mmekua wasikivu, mmeishi kwa ushirikiano, mmeishi kwa umoja na kuwa na nidhamu ya hali ya juu katika kipindi chote cha mafunzo yenu, mmedhihirisha kuwa ninyi ni viongozi wa kweli na mmekua katika misingi ya uongozi ndani ya CCM,” amesema Kawaida.
Aidha amewasisitiza kudumisha ushirikiano wa viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM na viongozi wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu katika maeneo yao.
“Ndugu viongozi niwasihi sana twendeni tukafanye kazi kwa ushirikiano sisi kwa sisi na tupendane mpaka watu waliopo nje washangae, lakini pia tushirikiane na viongozi wa serikali katika utekelezaji wa majukumu yetu kwenye maeneo yetu,” amesema Kawaida
Aidha, amesema kuwa ni vema viongozi hao wakafuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM na kutangaza kazi nzuri zinazofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika maeneo yao.
DAFTARI LA WAPIGA KURA
Amesema viongozi lazima wawe mstari wa mbele katika kuhamasisha vijana waweze kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa,vijiji na vitongoji 2024 na uchaguzi mkuu 2025.
“Sisi viongozi lazima tuwe mstari wa mbele katika uhamasishaji wa vijana kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025, twendeni tukawape hamasa ya kutosha vijana kujiandikisha kwenye Daftari la kudumu la wapiga kura na kushiriki kikamilifu katika chaguzi zote,” amesema
Mafunzo hayo yamefungwa na Mwenyekiti Kawaida, Ihemi mkoani Iringa ambapo awali yalifunguliwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi Julai 11, mwaka huu.