Tutamwambia mama’
Tunataka Bunge la bajeti lisimamie hoja za wananchi
Na MWANDISHI WETU
BUNGE ni Chombo cha uwakilishi wa Wananchi kama Ibara ya 62 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inavyotumika:
“Kutakuwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo litakuwa na sehemu mbili, yaani Rais na Wabunge. Rais kama sehemu moja ya Bunge atatekelezza yote aliyokabidhiwa na katiba hii. Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii”
Kimsingi, Bunge ni chombo cha uwakilishi wa wananchi. Kwa kuwa haiwezekani wananchi wote kukusanyika mahali pamoja na kufanya maamuzi muhimu katika uendeshaji wan chi, uwakilishi hauna budi kuwepo. Hii inamaanisha kwamba Wabunge wanapokuwa Bungeni hutekeleza majukumu yao kwa niaba ya wananchi.
Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge hufanya mikutano yake mara nne kwa mwaka mjini Dodoma, kutokana na hali hiyo tunaona sasa kesho Aprili 4, 2023 Bunge linaanza vikao vyake vya bajeti jijini Dodoma huku hoja kadhaa zikianza kuchakatwa kwenye kamati mbalimbali za kisekta.
Pamoja na hali hiyo bado tunabaki kwenye hoja ya msingi kwamba ni lazima wabunge wetu waende na kuisimamia Serikali yetu iweze kujadili juu ya kupanda kwa hali ya maisha na nafuu yake.
Tunajua utulivu wa dunia kwa kipindi cha miezi michache iliyopita haukuwa mzuri hasa kutokana na Vita vya Ukraine ambapo Taifa letu limeshuhudia mapito magumu kiasi cha kupanda kwa hali ya maisha kulikosabisha kupanda kwa bidhaa mbalimbali ikiwamo vyakula.
Ndio kama Watanzania tunabaki na wajibu wa kuendelea kuzishauri mamlaka mbalimbali likiwamo Bunge kwenda kukaa na kujadili kwa utulivu badala ya mihemko katika mapambano hayo dhidi ya hali ngumu ya Maisha.
Waswahili husema hili ni Bunge la kunyang’anyana shilingi kutokana, Tanzania ikikabiliwa na kupanda kwa bei za vyakula, wadau wamependekeza hatua tano muhimu zinazopaswa kuchukuliwa kunusuru hali hiyo.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji visivyo na kilevi ulikua kwa asilimia 9.7 katika mwaka unaoishia Desemba 2022 ukilinganisha na ilivyokuwa Desemba 2021.
Ongezeko hilo ni kubwa zaidi ukilinganisha na mfumuko wa asilimia 4.9 mwaka mmoja kabla. Mfumuko huu wa bei unachangiwa zaidi na ongezeko la bei ya vyakula kwa sababu asilimia 28.2 ya bidhaa zinazotumika kuandaa mfumuko wa bei ni vyakula na ndio bidhaa zinazochukua nafasi kubwa zaidi.
Kwa mujibu wa NBS, mfumuko wa bei wa jumla ulikua asilimia 4.3 mwaka 2022 ukilinganisha na asilimia 3.7 mwaka 2021 na asilimia 3.3 mwaka 2020.
Wadau mbalimbali wamekuwa wakishauri mbinu muhimu hasa kwenye ongezeko la bei za vyakula.Mathalan, gunia la kilo 100 la mchele linauzwa kwa wastani wa Shilingi 312,921 ukilinganisha na Shilingi 202,353 mwaka jana.
Gunia la maharage limefikia Shilingi 318,947, ongezeko la asilimia 55 ya ile ya mwaka jana iliyokuwa Sh203,118 kwa mujibu wa ripoti ya bei za vyakula ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.
Haya ni sehemu ya machache ambayo wabunge wetu wanapaswa kwenda kusimama ili kulisaidia Taifa ili kupunguza gharama za Maisha kwa Watanzania.
Tunajua kwamba Bunge ni sehemu ya uwakili hasa kwa wale ambao tumewachagua kwenda kusimamia hilo kwa maslahi mapana na waliowachagua ili kuinda maisha ya watanzania wanyonge.
Safu hii ya ‘tutamwambia mama’ tunaomba kuishia hapo ili kufikisha ujumbe kwa wawakilishi wa wananchi ambo sina shaka wengi wao tutashuhudia wakiwa kimya huku waliowachagu wakilia kwa ugumu wa maisha.