Na Mwandishi Wetu, Best Media
Benki ya NMB imetoa msaada wa vifaa tiba mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni tisa kwa Hospitali ya Wilaya ya Micheweni Pemba ikiwa ni utekelezaji wa azma yake ya kusaidia utoaji wa huduma bora za afya. Mchango wa benki hiyo unaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka huu.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mashuka 200, vitenganisha wodi 10, viti venye magurudumu vitano kwaajili ya kusaidia wagonjwa na mashine tatu za kupimia presha.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi msaada huo iliyofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Micheweni Pemba leo Jumanne Januari 3, 2023, Meneja wa NMB Tawi la Zanzibar, Naima Said Shaame alisema mchango wa benki hiyo unatokana na dhamira yake ya kusaidia ujenzi wa Taifa lenye afya bora.
“Sisi kama Benki ya NMB, tunaamini kuwa watu wenye afya njema wana tija hivyo wanaweza kushiriki katika mchakato wa kujenga taifa lenye afya bora. Kwa maana hiyo Benki kwa miaka saba iliyopita imekuwa ikishughulikia baadhi ya vifaa muhimu vya matibabu na ukarabati wa miundombinu kutoka kwa hospitali mbalimbali nchi ili kuboresha afya za wagonjwa. Mchango wetu kwa Hospitali ya Wilaya ya Micheweni leo ni ushuhuda wa hili,” amesema Shaame.
Shaame alisema benki yake inatoa kipaumbele kwa sekta ya afya nakusistitza kuwa sekta hiyo ni moja ya nguzo kuu za Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii wa benki hiyo na kuongeza kuwa benki hiyo inawajibika kwa asilimia moja ya faida baada ya kodi (PAT) kugharamia mipango mbalimbali ya kijamii katika maeneo yake ya kipaumbele ikiwemo afya, elimu na dharura.
Alisema Benki ya NMB imechangia kwa kiasi kikubwa katika hospitali mbalimbali nchini na kuongeza kuwa michango ya benki hiyo inaleta mabadiliko makubwa katika kuinua viwango vya utoaji wa huduma za afya nchini kote.
“Kama mbia wa maendeleo, tutaendelea kufanya kazi na Serikali na washirika wengine katika kuleta maendeleo yenye maana katika jamii tunazofanyia kazi,” amesema Shaame.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Mwinyi aliyepokea vitu hivyo kwa niaba ya Hospitali ya Wilaya aliishukuru benki hiyo kwa ukarimu wake na kuongeza kuwa uzinduzi wa Hospitali ya Wilaya ya Micheweni ni njia bora ya kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka huu.
“Hii ni miongoni mwa hospitali kumi ambazo tumepanga kuzizindua mwaka huu katika Wilaya zote zikiwemo Unguja na Pemba. Hatua itakayofuata ni kujenga hospitali za mikoa na tunatarajia kuanza na Mjini Magharibi Unguja na tutaendelea na mikoa mingine. Tutajenga hospitali ya Taifa Zanzibar na mara tu itakapokamilika, hakutakuwa na haja ya kuwahamisha wagonjwa kutoka Zanzaibar hadi Tanzania Bara au nje ya nchi,” amesema Dk. Mwinyi.
Aliwataka watoa huduma wa Hospitali hiyo ya Wilaya kutoa huduma bora na kuongeza kuwa huduma kwa wateja ni sehemu muhimu katika utoaji wa huduma za afya.
Waziri wa Afya Zanzibar Mhe, Nassor Ahmed Mazrui alisisitiza dhamira ya Wizara yake ya kutunza miundombinu katika Hospitali ya Wilaya ya Micheweni ili kutoa huduma bora za afya kwa Wazanzibari wote bila ya ubaguzi.