Na MWANDISHI WETU
-BEST MEDIA, MOROGORO
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amesikitishwa na ucheleweshwaji kwa kuanza kwa huduma ya Upasuaji katika Kituo cha Afya Mikese mkoani Morogoro wakati Serikali imeshatoa fedha Sh milioni 400 pamoja na kununua vifaa vyote muhimu vinavyohitajika lakini Halmashauri ya wilaya ya Morogoro Vijijini mkoani Morogoro imeshindwa kununua vifaa vidogo vilivyobakia ili wananchi wapate huduma hiyo.
Kutokana na hali hiyo pamoja na mambo mengine Katibu Mkuu Chongolo ameeleza kwamba ndani ya siku 14 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) atafika kwenye kituo hicho huku akimuagiza pia Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kukiangalia Wilaya hiyo kwa jicho tofauti kwani kwa hali inavyokwenda huduma hazitafika kwa wananchi kwa wakati.
Akizungumza baada ya kukagua kituo hicho cha afya na kujionea hali halisi ya ujenzi wa majengo yaliyojengwa na fedha iliyotumiwa na Serikali, Chongolo amesema amepita kwenye Wilaya nyingi za Tanzania na jana na leo amepita Wilaya ya Morogoro Vijijini ambapo kuna fedha nyingi zimepelekwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na mojawapo ni kwenye Kituo cha Afya Mikese ambapo limejengwa jengo la wagonjwa nje(OPD) na kupewa Sh milioni 400 kwa ajili ya kujenga majengo mengine.
“Na baada ya kutokamilika halmashauri ikaongeza Sh.milioni 60 lengo ni kufanikisha upatikanaji wa huduma bora, hapa Serikali imeshaleta vifaa tiba kwa asilimia 80 na iliyobakia ni kama asilimia 20 tu kukamilisha vifaa na kwa ajili ya kuanza kutoa huduma ya operesheni kuanza.Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini Mkuu wa Mkoa lazima muangalie kwa jicho la tofauti.
“Kwa namna hii hatutaweza kusaidia kufikisha huduma kwa wananchi ,tunatakiwa tukae kweli kweli kwa dhati ya mioyo yetu tuwe na wajibu kwa wananchi, niseme mbele ya wananchi sisi tumepewa dhamana ya kutengeneza na kuboresha mazingira ya huduma kwa wananchi na sio maneno.Hatuwezi kukaa mguu upande wananchi hawapati huduma halafusisi tukasema tunaraha tutakuwa hatutendi haki.
“Tumepewa dhamana kazi yetu ni kuhangaika na kufanya mambo yatokee sio hadithi, hapa (Mikese) mambo hayatokei na mimi naondoka nawaambia ndani ya mwezi mmoja mtaona mabadiliko, huwezi kwenda namna hii umma, wananchi unataka huduma, Serikali inaleta fedha hebu niambie haya majengo ya Thieta yamekaa muda mrefu hakuna anayetibiwa.
“Sasa kuna haja gani ya kujenga majengo mazurui kama haya, Rais Samia Suluhu Hassan anahaingaika kutafuta fedha huku na kule na wengine mpaka wanaanza kumsimanga kwa namna anavyohangaika kutafuta fedha.
“Hapa ameleta fedha Shilingi milioni 400 ijenge majengo, msaada wa haya majengo ni huduma sasa nani anachelewesha huduma?Ni watu wetu hapa hapa , hatuwezi kwenda namna hii , nitarudi Dar es Salaam naenda kukaa na Waziri wa TAMISEMI aje mwenyewe hapa ndani ya siku 14 aje ashuhudie haya, wameleta vifaa vya fedha nyingi imewekwa hakuna mtu anayehangaika,”amesema Chongolo.
Ameongeza vifaa vilivyopelekwa na Serikali kwenye kituo hicho ni kwa ajili ya wananchi kutumia lakini havitumiki halafu wao(CCM)wakija wanasema kidumu Chama Cha Mapinduzi… kitadumu mambo yakinyooka.“Hakiwezi kudumu tukiwa sisi wenyewe tunajihujumu, haiwezekani hata kidogo, nimepewa kazi ya kuwa Katibu Mkuu wa Chama siwezi kuja nikaona mambo ya hovyo nikapiga makofi .
“Nitakuwa simtendei haki aliyenipa dhamana hii Mwenyekiti wangu wa Chama ambaye ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunakuja kukagua utekelezaji wa Ilani na tukija tukiona mambo hayaendi na ninyi mtatushangilia baadae.Hivi ninyi mnaona tuko kwenye mkao wa kushangiliwa kwenye mambo yasiyokuwa na maana? Hili halikubaliki, taa iko tayari, vitanda viko tayari, hivyo vifaa vya milioni 200 unataka kufunga nini? Hii mnipe kazi ya kufuatilia ili kifuatacho kuwe na uhakika wa kufanya operesheni.
“Nami naenda kujifunza lakini niwahakikishe ikifika Machi mwaka huu watu wataanza kufanyiwa operesheni kama kuna changamoto kwenye uzazi.Naondoka nitakaa wiki nne nitakuja hapa tuje tuone tulichokubaliana na kilichofanyika na kama mtakuwa na changamoto basi mfuate taratibu, sheria na kanuni lakini jambo lilite matokeo.”
Chongolo amesema vifaa tiba vilivyobakia ni vidogo na vifaa vilivyopo haviwezi kukaa bila kutumika na watu wanatakiwa kupata huduma , hiyo haileti picha nzuri huku akifafanua wanapita kwenye korido kitanda kimewekwa tu tena kikiwa na godoro jipya , hiyo haileti tija.
“Tunahaingaika kupunguza vifo vya mama na mtoto , watu wote wangetamani kuona kila kifaa kinachowekwa maana kifaa unachokiona ni fedha ya Serikali imetumika.Nisikilizeni mimi ni Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ndio mtendaji wake mkuu na wapo wengine ambao ndio wasaidizi wake kwenye idara mbalimbali ndani ya Chama.
Rais Samia Suluhu Hassan anahangaika na anakesha ni kutafuta fedha za kutatua changamoto za wananchi, ana hangaika kufafuta ili zilete mabadiliko kututoa tulikokuwa kwenda hatua nyingine. Mahali kwenye changamoto tuseme hapa hatujaridhika tunatamani kuona tunavuka kwenda hatua nyingine.
“Tunataka kuona ile Thieta inafanya kazi haraka , hakuna kigezo cha msingi cha kushindwa kufanya kazi na kama uzoefu wameshaupata warudi hapa kwenye kituo chao cha kufanya kazi , kwa hiyo watu tunategemea wapatiwe huduma ya upasuaji hapa hapa kwasababu vifaa Serikali imeshaleta vilivyobakia ni kidogo na hawa mabwana(Halmashauri) wana fedha ya kununua vidogo vilivyobakia ili kazi ya operesheni ianze hapa,”amesema Chongolo.