TUME ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeshauriwa kuongeza juhudi katika kuelimisha walimu juu ya haki na wajibu katika utumishi wao ili kuhakikisha hawakatishi ajira zao kutokana na kuchukuliwa hatua kwa kukiuka Miiko na Maadili ya kazi hiyo.
Ushauri huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Afisa Elimu Msingi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Dk. Ruth Kulang’wa wakati akifunga mafunzo ya siku tatu mjini Shinyanga ambayo yaliandaliwa na TSC kwa ufadhili wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya World Vision Tanzania.
Mafunzo hayo yaliyowakutanisha Wenyeviti wa Kamati za TSC, Watumishi wa TSC, maofisa Elimu, Wathibiti Ubora wa Shule na Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Wilaya za Mikoa ya Shinyanga, Tabora na Simiyu yalilenga kuandaa wakufunzi watakaotoa elimu kwa walimu katika ngazi ya shule juu ya masuala ya Ajira na Maadili katika Utumishi wa Walimu pamoja na wajibu wa jamii katika kumlinda na kumlea mtoto katika Maadili Mema.
Dk. Kulang’wa amesema mwalimu amepewa jukumu kubwa la kumtengeneza mtoto na kumwandaa kuwa raia mwema na mwadilifu kwa manufaa ya Taifa, hivyo kutokana na wajibu huo ni vyema TSC iendelee na jukumu la kuwakumbusha walimu juu ya maadili na miiko ya kazi yao mara kwa mara na kuhakikisha wototo wanakuzwa katika maadili yanayohitajika.
“Napenda kuwapongeza TSC kwa kuwa na wazo la kuandaa andiko la kuwafikia walimu na kuwakumbusha kuhusu maadili, wajibu pamoja na haki zao. Vilevile, ninapenda kuwapongeza World Vision Tanzania kwa kuona umuhimu wa kumsaidia mwalimu kupitia TSC ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo,” amesema Afisa Elimu huyo.
Amefafanua kuwa pamoja na kupewa jukumu hilo kubwa, kuna walimu wapo kazini hawaelewi kabisa kama kuna wajibu unaowataka wautende kwa jamii, kwa walimu wenzao na hata kwa watoto, hivyo ni rahisi kujikuta wamefanya mambo ambayo ni kinyuime na taratibu na kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.
“Ni vizuri tuelewe kwamba Serikali haina dhamira ya kuwafukuza kazi walimu wake, sisi wadau wa elimu tunapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha tuwasaidia walimu wasikiuke masharti ya kazi. Tuwasaidie kutambua Kanuni za Utumishi wa Walimu na madhara ya kwenda kinyume na kanuni hizo ili wajiepushe na makosa,” amesema Kulang’wa.
Kuhusu kumlinda mtoto dhidi ya ukatili, Ofisa Elimu huyo amesema kuwa jukumu la mwalimu haliishii katika kufundisha mwanafunzi peke yake, bali ana wajibu wa kuelimisha wazazi na jamii kwa ujumla kuhusu kulinda mtoto dhidi ya ukatili anaofanyiwa ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii yatakayotokomeza kila ina ya ukatili na kufanya kila mtoto aweze kutimiza ndoto zake bila kukatishwa.
Ameleza kuwa pamoja na wajibu kuna haki za mwalimu ambazo zipo kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Walimu na Utumishi wa Umma lakini walimu hawazijui na wakati mwingine hawazipati, hivyo amewasihi Maafisa Elimu, Wathibiti Ubora wa Shule pamoja na Watendaji wa TSC kuwasaidia walimu kutambua na kupata haki zao kwa wakati badala ya kuwa kikwazo kwao.
“Katika mafunzo haya, tumefundishwa majukumu ambayo mwalimu anayo kwa mtoto, kwa jamii, kwa mwajiri na kwa walimu wenzake, lakini pia kuna haki na wajibu wa mwalimu. Hapa kwenye haki kuna vitu vingi ambavyo walimu hawavijui, na sisi ndiyo wenye wajibu kufanya walimu wazitambue na wazipate kwa wakati. Ninaomba kila mmoja aone kwamba amepewa jukumu kubwa la kufanya katika kusaidia walimu wafanye kazi katika mazingira bora ili aweze kuhudumia watoto kwa bidii, weledi, ufanisi na uzalendo,” amesema.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Fatuma Muya amesema washiriki walijengewa uwezo katika masuala mbalimbali ikiwemo; Haki na wajibu wa mwalimu katika kazi yake, Maadili ya kazi ya ualimu, Mamlaka ya nidhamu kwa mwalimu, Utaratibu wa ajira kwa walimu, Muundo wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Nidhamu katika Utumishi wa Walimu, Uendeshaji wa Vikao vya Kamati za TSC Wilaya pamoja na Majukumu na Malengo ya Taasisi ya World Vision Tanzania.
Muya amesema washiriki hao walipata fursa ya kufanya kazi kwa vitendo katika vikundi ili kuwapima uelewa wa kile walichofundishwa kwa kuwa wanatarajiwa kwenda kuwajengea uwezo walimu katika ngazi ya shule.
“Tunamshukuru Mungu Mafunzo yamekwenda vizuri, mada zilizowasilishwa zimeeleweka vizuri kwa washiriki, tumewapatia kazi za vikundi na hatimaye wamefanya mawasilisho ya namna watakavyotekeleleza kazi hiyo kwa walimu wetu. Tunaamini elimu hii itakuwa ni chachu ya kuleta mabadiliko kwa walimu wetu na jamii kwa ujumla ili shule zetu ziwe mahali salama kwa watoto,” alisema Muya.
Naye, mwakilishi kutoka Taasisi ya World Vision Tanzania, Zacharia Nyandekwa amesema wamefandhili mafunzo hayo kwa kuwa Tume ya Utumishi wa Walimu ina malengo yanayoendana na Taasisi hiyo katika kuimarisha nidhamu kwa walimu ili watoto waweze kupata haki yao ya kufundishwa na kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na ukatili.
“Niwaahidi kwamba sisi World Vision huu ni mwanzo, tunaona malengo yatu na ya TSC yanaendana, lengo kubwa ni kuwa maadili yawe mazuri shuleni na kwa jamii nzima kwa ujumla ili watoto wetu wawe salama zaidi. Tunamini kwamba World Vision Tanzania tukifanya kazi kwa ushirikiano mzuri na TSC tutaifanya Tanzania yetu iwe salama,” amesema Nyandekwa.
Ameongeza kuwa World Vision Tanzania inaunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kutokomeza vitendo vyote vya udhalilishaji wa watoto pamoja na jitihada za kuwaondolea wananchi umaskini, hivyo ameahidi kutoa ushirikiano kwa ofisi za Tume hiyo zilizopo kwenye Wilaya ambazo taasisi hiyo inafanya kazi.
“Tumeanza na mafunzo ya siku tatu hapa, lakini pia kadiri siku zinavyokwenda tutafanya mambo makubwa zaidi. Na kwa kutambua umuhimu wa mafunzo haya, tumezalisha nakala za kitini cha mwongozo wa kutolea mafunzo ambapo kwa kuanzia tutagawa vitini vinne kwa kila shule,” amesema Nyandekwa.