KIKOSI cha Yanga SC kimesafiri kuelekea nchini Tunisia kupitia Dubai kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF CC) dhidi ya US Monastir ya nchini humo, mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Olympic Stadium of Rades (Stade Hammadi Agrebi) jijini Tunis, Februari 12, 2023.
Katika mchezo huo dhidi ya US Monastir ya Tunisia, Yanga SC wameondoka nyumbani nchini Tanzania wakiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye mtanange huo wa kwanza wa Kundi D la Michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kabla ya safari ya kuelekea Tunisia, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ally Kamwe amesema wanatambua umuhimu wa alama tatu katika kila mchezo wa Kundi hilo lenye timu za US Monastir ya Tunisia, TP Mazembe ya DR Congo na Real Bamako ya Mali.
Hata hivyo, baada ya mchezo huo dhidi ya US Monastir, Wananchi watakuwa na kibarua kizito Februari 19, 2023 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya miamba ya soka nchini DR Congo, TP Mazembe ikiwa ni mchezo wa pili wa Kundi D la Michuano hiyo ya CAF CC.
“Hii siku ya Jumapili dhidi ya TP Mazembe ni muhimu sana, na tumeipa jina maalum, ‘Wananchi Super Sunday’ maana ndio utakuwa mchezo mkuwa barani Afrika kwa hiyo siku ya Jumapili,” amesema Ally Kamwe.