Home MICHEZO TAMASHA LA SAUTI ZA BUSARA MSIMU WA 20 KUANZA RASMI LEO ZANZIBAR

TAMASHA LA SAUTI ZA BUSARA MSIMU WA 20 KUANZA RASMI LEO ZANZIBAR

Google search engine

Na Andrew Chale

-BEST MEDIA, ZANZIBAR

MJI wa Unguja na viunga vyake unatarajiwa kupamba moto  kwa muziki ‘mnene’ kutoka kwa wasanii nguli wa Kitaifa na Kimataifa ambao watatumbuiza kwa siku tatu kuanzia leo 10 hadi 12 Februari ndani ya Ngome Kongwe.

Wapenda burudani kutoka maeno yote ya dunia, watashuhudia baada ya miaka 19 ya mafanikio, Sauti za Busara, moja ya matamasha bora barani Afrika.

Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari, mjini hapa leo, Mkurugenzi wa Tamasha hilo, Yusuf Mahmoud ‘Dj Yusuf’ amebainisha kuwa, leo ni siku ya kwanza kati ya siku tatu za kusherehekea muziki wa Kiafrika na utofauti wa kiutamaduni huku wasanii mbalimbali kutoka barani Afrika wakipamba katika majukwaa mawili.

‘’Leo Ijumaa Februari 10 katika eneo la Ngome Kongwe, Stone Town, Sauti za Busara  itashuhudia msimu wa 20 tangu kuanzishwa kwake.

Ni fursa ya kipekee kwa kikundi cha DCMA Young Stars, ambao ni watoto wadogo wenye vipaji kutoka shule tofauti visiwani Zanzibar kutarajiwa kutumbuiza na wanamuziki na walimu kutoka Chuo cha Muziki cha Dhow Countries cha Zanzibar.

Aidha, Yusuf Mahmoud amewataka Watanzania kujumuika na wageni wengi ambao tayari wamefika kutoka kila pembe ya dunia kushuhudia na kushiriki katika tamasha hilo la kipekee.

“Leo, tunaanza kwa uzoefu wa kipekee na wa ajabu wakati Zanzibar ikiandaa siku tatu zitakazobeba asilimia 100 ya muziki wa Kiafrika. 

Tunajivunia kwa mwaka huu kuadhimisha tamasha la 20, tukiwa na orodha bora zaidi ya wanamuziki itakayowaridhisha wahudhuriaji kutoka katika kila kona ya dunia,” amesema Yusuf Mahmoud.

Kwa mujibu wa Bw. Mahmoud, miongo miwili ya burudani imefanya Sauti za Busara kuwa moja ya matamasha yanayoheshimika zaidi ya muziki wa Kiafrika ambayo imeendelea kufanyika, hata katika miaka yote ya changamoto ya janga la Uviko-19.

“Kwa miongo miwili sasa, tumeonyesha uthabiti na wepesi katika kusaidia wasanii, huku tukisisitiza nguvu na ushawishi wa muziki itumike kukemea ya maovu katika jamii yetu.

Kwa kutambua ukweli kwamba Afrika ni bara kubwa lenye historia na tamaduni tofauti na matarajio ya pamoja, onyesho la mwaka huu linafanyika chini ya kaulimbiu ‘Utofauti Wetu ni Utajiri Wetu.’’.

Kwa upande wake, Meneja wa tamasha hilo, Journey Ramadhan aliwataja baadhi ya wasanii ambao maonyesho yao yaliacha gumzo kwa miongo miwili iliyopita.

“Tumeandaa matamasha na kuwa na mamia ya vikundi, lakini kuna wale amabo wmeacha gumzo kwa mfano, mwanamuziki mkongwe kutoka Zanzibar Marehemu Bi Kidude, Sampa The Great (Zambia), Nneka (Nigeria), Bassekou Kouyate (Mali), Blitz the Ambassador (Ghana), Sarabi (Kenya), Samba Mapangala (DRC), Ba Cissoko (Guinea), Sholo Mwamba, Saida Karoli na Jagwa Music (Tanzania) wanamuziki hawa walipendwa na karibu kila mtu,” alisema Journey Ramadhan.

Kwa upande wake Alfred Vendeline kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa CPS-Fumba Town, Sebastian Dietzold alisema wanajivunia kuwa sehemu ya tamasha kubwa zaidi la muziki barani Afrika ambalo kwa miaka mingi limeacha kumbukumbu za kudumu.

“Jinsi Sauti za Busara inavyoleta watu mbalimbali kutoka nchi mbalimbali kusherehekea muziki wa tamaduni mbalimbali, Fumba Town pia inawaleta pamoja watu kutoka nchi na tamaduni mbalimbali kununua na kufurahia nyumba za makazi na likizo za bei nafuu Zanzibar,” alibainisha.

‘’Kesho Jumamosi Februari 11, mchana katika Mji wa Fumba, mradi ulio chini ya CPS, kutakuwa na burudani ya kipekee kwa wasanii mbalimbali wakiwemo Sitti and the Band. 

Usafiri utakuwapo Ngome Kongwe wa kwenda na kurudi kila baada ya nusu saa kuanzia saa Nne asubuhi hadi saa 10 jioni.

Fumba Town, tumejiandaa kuonesha tamaduni, tofauti pale wanaishi watu wa mataifa mengi na wote watafurahia tamasha hili ambalo tunaliita Busara Plus’’. Alisema.

Aidha, Tamasha la mwaka huu pia litakuwa na Movers & Shakers (jukwaa lisilo rasmi la kubadilishana uzoefu la wataalam mbalimbali), Swahili Encounters (ushirikiano wa wanamuziki wa hapa nchini na wageni), maonyesho ya Busara Plus katika Mji wa Fumba na maeneo mengine, na Tuzo ya Emerson Zanzibar Music Award, kwa wanamuziki wa hapa nchini.

Tamasha la mwaka huu limefadhiliwa na wadhamini mbalimbali ikiwemo ufadhili wa Fumba Town- CPS,CRDB bank, Ignite Culture, Ubalozi wa Australia, Ubalozi wa Ufaransa, Institut Français, Kendwa Rocks, 

Adventure247 Marketing Agency, Mjini FM, ST Bongo TV, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Zanzibar Serena Hotel, Coconut FM, Zanlink, Emerson Zanzibar, 2Tech Security na wengine wengi.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here