Na Muhidin Amri,Tunduru
SERIKALI ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma, imesema itawakamata na kuwatoza faini kubwa wafugaji wote wanaoishi kiholela na kuchunga mifugo nje ya maeneo yaliyotengwa (vitalu).
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa wilaya hiyo, Julius Mtatiro wakati akizungumza na wafugaji wakati wa ufunguzi wa nyumba ya kulala wageni ya Kajima Guest House iliyojengwa na mfugaji wa jamii ya Kisukuma Mahembo Shamba.
Mfugaji huyo amelazimika kuuza sehemu ya mifugo yake na kujenga nyumba ya kulala wageni, ikiwa ni utekelezaji wa agiza la serikali linalowataka wafugaji kupunguza mifugo na kuwekeza kwenye miradi mingine ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Mtatiro, licha ya mapenzi makubwa ya serikali kwa jamii ya wafugaji wilayani humo, lakini bado kuna wafugaji wanakahidi na kufanya ufugaji kiujanja ujanja kwenye makazi ya wakulima na kusababisha migogoro mingi kati ya makundi hayo mawili.
Amesema, Wilaya ya Tunduru ni ya kilimo licha ya kukaribisha wafugaji, hata hivyo suruhisho la migogoro inayojitokeza kati ya wakulima na wafugaji ni lazima wafugaji wakapelekwa katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli zao.
Mtatiro, amempongeza mfugaji huyo kwa kuitikia wito wa serikali kwa kupunguza idadi ya mifugo yake na kufanya uwekezaji wa nyumba ya wageni na kuwataka wafugaji wengine kuiga mfano huo.
Kwa upande wake mfugaji huyo amesema,amelazimika kujenga nyumba ya wageni baada ya kupoteza sehemu kubwa ya mifugo yake mkoani Mbeya na Morogoro na amelazimika kuja wilayani Tunduru baada ya kusikia kuna mazingira mazuri kwa ajili ya kuchungia.
Amesema, hadi kukamilika kwa nyumba hiyo yenye vyumba 10 vya kulala wageni ametumia fedha nyingi baada ya kuuza ng’ombe 220 na kuwataka wafugaji wengine kupunguza mifugo yao na kuwekeza katika miradi mingine ya kiuchumi.