WATANZANIA 170 watakaohusika katika ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima – Uganda hadi Chongoleani Tanga (EACOP), wamepatiwa mafunzo maalum yakayayowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi katika mradi huo.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni ya EACOP yamezinduliwa tarehe 15 Februari, 2023, jijini Tanga na Kamishna wa Petroli na Gesi, Michael Mjinja kwa niaba ya Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba.
Akizindua mafunzo hayo, Mjinja amesema kuwa, mafunzo hayo yatawawezesha Watanzania hao kufikia viwango na sifa za kutambulika kimataifa katika ujenzi wa miundombinu ya Mafuta na Gesi hivyo aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia ujuzi huo watakaoupata si tu kitaifa bali pia kimataifa.
Mjinja amesema “kupatikana kwa fursa hizi za mafunzo, ujuzi, elimu na ajira ni sehemu tu ya juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kufungua milango kwa Watanzania ili kuwawezesha kuingia katika soko la ajira hapa nchini na katika Jumuiya za Kimataifa kama anavyofanya katika sekta nyingine hapa nchini.”
Amewahimiza watanzania hao kushiriki katika mafunzo hayo na ujenzi wa mradi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa. Pia amevitaka vyuo vinavyotoa mafunzo hayo kuweka kumbukumbu za wahitimu wa mafunzo hayo na kufanya mawasiliano na Wizara ya Nishati ili Wizara iweze kuwafuatilia pale fursa nyingine zinapojitokeza ndani na nje ya nchi.
Mjinja, ameeleza zaidi kuwa, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kimsingi katika ujenzi wa Bomba la Mafuta ikiwemo kutenga baadhi ya kazi na huduma katika mradi zifanywe na Watanzania pekee. Aidha, amesema Serikali imeendelea kuwajengea Watanzania uelewa kuhusu mradi ili watanzania wengi zaidi waweze kushiriki.
Ameongeza kuwa, hadi sasa takribani kampuni 146 za Kitanzania na Watanzania zaidi ya 1,600 wameweza kushiriki katika mradi. Aidha, Serikali imeendelea kuwekea mkazo suala la kuwaendeleza Watanzania kwa kuhaulisha utaalamu.
Ametanabaisha kuwa, mradi huo wa Bomba la Mafuta unatekelezwa na utatekelezwa kama ulivyopangwa kwa kuzingatia taratibu na sheria za nchi na taratibu za Kimataifa.
Ameishukuru Kampuni ya EACOP na Uongozi wa Mkoa wa Tanga kwa kushiriki kikamilifu katika utoaji wa mafunzo hayo na kuahidi kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na Kampuni ya EACOP pamoja na Wakandarasi wake katika kutoa mafunzo kama hayo kwa Watanzania hadi hapo mradi utakapokamilika.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Dk. Japhet Simed ameishukuru Wizara ya Nishati kwa uratibu wa mradi huo kuanzia mwanzo hadi hatua iliyofikiwa na kusema kuwa, ajira nyingi zaidi zinatarajiwa kupatikana kwa wakazi wa mkoa wa Tanga na watanzania wote kiujumla.