Na MWANDISHI WETU
-BEST MEDIA, MOROGORO
WANANCHI wametakiwa kujiunga na Bima mbalimbali ili kukabiliana na majanga ikiwemo ya moto ikiwa ni kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan
Rai hiyo ilitolewa na Kaimu Meneja wa Benki ya NMB kanda ya Kati, Harold Lambileki wakati wa uzinduzi wa kampeni ya benki hiyo ya ‘umebima’ Mjini Morogoro katika soko la Kingalu kwa lengo la kuwahamasisha wananchi kujiunga na bima ili kujiongezea hali ya kujiamini katika utendaji wa kazi na maisha kwa ujumla.
Lambileki amesema kuwa benki ya NMB kwa kutambua umuhimu wa bima kwa watanzania na kutokana na mazingira yaliopo kwa sasa kwamba watanzania wengi bado hawajajiunga na mfumo huo hivyo wamelazimika kuhamasisha watanzania kujiunga na bima kupitia matawi ya benki hiyo yaliopo kote nchini.
“Kwa kushirikiana na makampuni kumi tofauti ya Bima hapa nchini, mteja hata asiye wa NMB anaweza kufika katika matawi yetu na kujikatia bima katika kampuni yeyote kati hizo kumi ambazo tunafanya nazo kazi kwenye bima ya afya, maisha, majanga, elimu na bima ya faraja kwa vikundi” alisema Lamibileki.
Aidha, baadhi ya wanufaika wa benki hiyo, Paul Simya na Martin Joseph Msungwa walielezea umuhimu wa kujiunga na bima ili kukabiliana na majanga mbalimbali ikiwemo ajali pamoja na moto hasa ukizingatia vijana wengi kwa sasa wamejiajiri kwenye biashara ya usafirishaji abiria kwa bodaboda na Bajaji.
“Mimi ni mnufaika na benki ya NMB iliweza kupata mkopo wa bajaji kisha nikajiunga na bima ambayo ninaamini itanisaidia katika kukabiliana na majanga mbalimbali pindi yatakapojitokeza.” amesema Simya.
Kwa upande wake Martin Joseph aliwahamasisha vijana wenzake kutopuuza kujiunga na bima ili kupunguzia changamoto ya matibabu katika ngazi ya familia na wao wenyewe kwa kuwa taifa linawategemea vijana kwenye uzalishaji.
Benki ya NMB kwa sasa inatimiza miaka 25 toka ianze kutoa huduma zake kwa jamii hivyo wamekuja na kampeni mbalimbali ikiwa ni kuwaleta wananchi kwa pamoja kutambua huduma wanazozitoa huku wakiwa na kauli isemayo umebima, teleza na hii.