NA MWANDISHI WETU
WASHINDI 7 wa kampeni ya kuhamasisha matumizi ya kadi iliyoondeshwa na Benki ya NMB ‘NMB MastaBata – Kote Kote’ wameagwa na kukabidhiwa tiketi za safari yao ya Dubai iliyolipiwa gharama zote, na tayari wamendoka nchini jana mchana.
Hafla ya makabidhiano na kuwaaga washindi hao na wenza wao, imefanyika Makao Makuu ya NMB, ambapo walikabidhiwa tiketi zao na Mkuu wa Idara ya Kadi ya NMB, Philbert Casmir.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Casmir alisema kwamba malengo matatu ya kampeni hiyo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa, huku akiyataja kuwa ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya kadi, ambayo ni rahisi, nafuu na salama zaidi, kuliko matumizi ya pesa taslimu, ambayo ni hatarishi na ya gharama kubwa.
“Malengo mengine ya NMB MastaBata yalikuwa ni kurejesha kwa wateja sehemu ya faida jambo linalothibitisha namna tunavyowajali, lakini pia kampeni ililenga kuthibitisha uimara wetu katika masuluhisho ya kidijitali, ambako NMB tumefanya uwekezaji mkubwa.
“Katika hili, NMB tumeshirikiana na MasterCard na tunawatakia washindi wetu ambao wataongozana na maafisa wa benki yetu safari njema, ambayo tunaamini itakuwa na siku nne zenye mambo mengi ya kujifunza, ikiwemo fursa za kibiashara na utalii,” alisema Casmir.
Aliongeza ya kwamba, mwisho wa NMB MastaBata ‘Kote Kote’ iliyoanza Oktoba 28 mwaka jana, ni mwanzo wa kampeni nyingine mbalimbali, huku akiwataka Watanzania na wateja wa NMB kukaa mkao wa kuchangamkia kila fursa inayokuja kupitia huduma za benki hiyo.
Washindi na wafanyakazi wawili waliokabidhiwa tiketi na kuondoka jana mchana ni pamoja na Rose Qamara, Upendo Msanjila, Edwin Mwakabage, Nazia Lakha, Xaveria Hyera, Chintan Kamania na John Lubisha.
Akizungumza kwa niaba washindi hao, Upendo Msanjila alikiri kufurahishwa sana na safari hiyo, ambayo awali wakati akipigiwa simu ya ushindi hakuamini akihisi ni matapeli na kwamba NMB imewezesha kwa mara ya kwanza yeye kutembelea Dubai akiwa na mwenza wake.
Naye John Lubisha, alielezea kiwango cha juu cha furaha yake kwa kushinda moja kati ya nafasi saba zilizokuwa zikishindaniwa na wateja zaidi ya Milioni 5 benki hiyo katika kipindi cha miezi mitatu iliyojumuisha zawadi zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 350.