Home KITAIFA NMB yaanzisha huduma ya mikopo nafuu  ya elimu

NMB yaanzisha huduma ya mikopo nafuu  ya elimu

Google search engine
Mkurungenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimi ya Juu,   Abdul-Razaq Badru akimpongeza Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB ,Ruth Zaipuna (watatu kulia) mara  baada ya uzinduzi  wa mikopo ya elimu ya Juu hapa Nchini inayotolewa na benki ya NMB. Benki ya NMB imetenga  sh bilioni 200 kwa ajili ya mikopo hiyo kwa mwaka huu. uzinduzi huo ulifanyika jana Jijini Dodoma ,wengine katika picha kushoto ni Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia ,Prof Aldof Mkenda na wapili kulia ni Afisa Mkuu wa wateja binafsi na biashara,Filbert Mpozi mwisho ni Meneja wa NMB Kanda ya Kati,Nsolo Mlozi.

Na Mwandishi Wetu

Benki ya NMB imesema imetenga kiasi cha TZS bilioni 200 kwa ajili ya kuwakopesha wafanyakazi wanaotaka kupata elimu ya juu au wale wanaohitaji fedha za kuwasomesha wategemezi wao.

Bidhaa hiyo mpya ya mikopo nafuu inayoleta ahueni kubwa katika ufadhili wa hasa elimu ya juu nchini ilizinduliwa rasmi jana jijini Dodoma na tayari inapatikana kwenye matawi yote ya benki hiyo yaliyotapakaa nchi nzima.

Mbali na vyuo vikuu, huduma ya ufadhili huu ambayo jina lake la kibiashara ni NMB Elimu Loan itatolewa pia kwa ngazi zote za elimu zikiwemo shule za msingi na secondari hata vyuo vya ufundi.

Akitangaza kuanzishwa kwake rasmi, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna, alisema mikopo inayotolewa kwa mwajiriwa yeyote inaanzia TZS 200,000 hadi TZS milioni 10 kwa mwaka kwa mtu mmoja.

Zaipuna alibainisha kuwa moja ya sifa za kupata mkopo huo, wenye riba ya asilimia tisa tu na ambao marejesho yake ni ndani ya miezi 12, ni kuwa mwajiriwa ambaye ni mteja wa NMB.

“Kuanzia leo (Jumanne), tumeanza rasmi kupokea maombi ya mkopo kwa ajili ya kugharamia elimu kwa wafanyakazi ambao mishahara yao inapita Benki ya NMB,” kiongozi  huyo aliwaambia waliodhuria hafla ya uzinduzi wa ufadhili huo mkubwa kuwahi kuwepo nchini ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda,

“Huu ni  utekelezaji wa makubaliano yetu na Wizara ya Elimu ya kuanza kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kupunguza utegemezi wa  waajiriwa kwa bodi ya mikopo (HESLB) pale wanapotaka kujiendeleza kimasomo na pia kuwalipia ada vijana wao,” alifafanua.

Aidha, alisema kuwa NMB ina dhamira ya dhati katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha tasnia ya elimu na kuchangia kutoa elimu bora kwa wote huku ikiwa mstari wa mbele kupanua wigo wa upatikanaji wa fedha za kuwafadhili wote wanaohitaji kujiendeleza kielimu.

“Tumezindua huduma hii hapa Dodoma leo lakini mikopo hii inatolewa katika matawi yetu yote nchi nzima,” afisa huyo alibainisha na kusema fedha zitakazotolewa zitaingizwa moja kwa moja katika akaunti ya shule au chuo husika na wala si vinginevyo.

“Ili kupata mkopo huu, fika tawi lolote la NMB na nakala ya mshahara wako, mtiriko wa ada, barua ya kujiunga na chuo na wafanyakazi wa Benki ya NMB watakupigia hesabu ya mkopo unaostahili kupata,” CEO Zaipuna alidokeza wakati akiyataja masharti ya kukopeshwa.

Kwa kuanzisha huduma hii, NMB inakuwa imetimiza ahadi iliyoitoa mwaka jana yakuisaidia Serikali kuipunguzia HESLB mzigo wa kufadhili masomo ya juu na kuwa na vyanzo vipya vya mikopo ya elimu.

Mwishoni mwa mwaka jana, benki hiyo ilifanya makubaliano na Serikali kupitia Wizara ya Elimu ya kuanza kuwakopesha wazazi kwa riba nafuu ili waweze kugharamia elimu yao ya juu au kuwasomesha wategemezi wao.

“Yote haya yanalenga  kuendeleza juhudi za kukuza sekta ya elimu hapa nchini, na sisi kama wadau wakuu wa elimu, tumeona tutoe ushirikiano huu kwa serikali kwa manufaa ya watanzania wenzetu,” Bi Zaipuna alibainisha huku akisisitiza kuwa NMB itaendelea kubuni suluhishi zaidi za kuboresha elimu na kuimarisha tasnia hiyo.

Katika hotuba yake, Waziri Mkenda aliweka bayana matamanio yake ya kutaka kupatikana ufadhili zaidi ya kile ilichokifanya NMB kutoka kwa wadu wengine.

Aidha, alisema kuwa uwekezaji wa NMB ni kitu kikubwa kinachoongeza wigo wa watu kujisomesha na akaomba hela za mikopo hiyo zitumike kwa ajili ya madhumuni yaliyokosudiwa tu.

Waziri huyo alisema pamoja na bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kuongezeka kutoka TZS bilioni 464 Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani hadi TZS bilioni 657 kwenye mwaka huu wa fedha bado kuna uhitaji wa vyanzo vingine kama hiki kipya kilichoanzishwa na NMB.

“Nikiri kuwa nyie ni wadau wa kweli wa elimu nchini na mmeonyesha njia inayostahili kuzingatiwa na wadau wengine,” Prof Mkenda alisisitiza.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof Carolyne Nombo alisema NMB ni zaidi ya mdau kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya elimu hasa kupitia ubunifu wake mkubwa pamoja na michango ya hali na mali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Profesa Kitila Mkumbo, alisema uzinduzi wa huduma mpya uliyofanywa na NMB ni muhimu sana kwani fedha za mikopo kwa ajili ya wanafunzi hazijawahi kutosha.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here