Na Mwandishi Wetu
BENKI ya NMB imetoa msaada vifaa mbalimbali kwa sekta za elimu na afya vyenye thamani ya shilingi milioni 39 kwa Wilaya za Kanda ya Kati zikiwemo Mpwapwa, Kondoa na Chemba ikiwa ni utekelezaji wa sehemu ya dhamira yake ya kurudisha kwa jamii.
Walionufaika katika Wilaya ya Mpwapwa ni pamoja na Shule za Msingi Iyoma na Mpwapwa zilizopokea madawati 100 kwa jumla yenye thamani ya shilingi milioni 10.
Walionufaika katika Wilaya ya Kondoa kwa upande mwingine ni pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Kondoa ambayo iliyopokea mashuka 200 yenye thamani ya shilingi milioni 6m, Shule za Sekondari Bicha, Masange, Kimaha na Dalai zilizopokea meza na viti 50 kila moja vyenye thamani ya shilingi milioni 5 huku Shule ya Msingi Lembo ikipata vifaa vya kuezekea vyenye thamani ya shilingi milioni 5.6.
Kwa upande wa sekta ya afya, benki hiyo pia ilitoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 12.3 katika Hospitali ya Wilaya ya Chemba ambavyo ni pamoja na mashuka 64, vitanda vya kujifungulia vinne, vitanda vya kawaida vya wagonjwa 10, na magodoro kumi miongoni mwa vifaa hivyo kwa lengo la kuasaidia kuimarisha utoaji huduma hospitalini hapo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi msaada huo, Meneja wa Kanda ya Kati wa Benki ya NMB, Nsolo Mlonzi alisema msaada huo unathibitisha dhamira ya benki hiyo ya kurudisha kwa jamii inapofanyia kazi na kuongeza kuwa benki hiyo imetenga shilingi bilioni 6.2 kusaidia uwekezaji katika uwekezaji katika miradi mbalimbali ya ya kijamii hususan katika sekta zake za kipaumbele ikijumuisha elimu, afya na dharura mwaka huu.
“Katika Benki ya NMB, elimu na afya ni vipaumbele vyetu muhimu kwani tunaamini elimu ni ufunguo wa maisha bora ya baadaye ya watoto, lakini bila vifaa vya kutosha, watoto wengi hupata shida kujifunza. Kama wadau wakubwa wa maendeleo, leo tunakabidhi madawati na meza ili kuimarisha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wetu,” Mlonzi alisema.
Wakati wa hafla hiyo Mlonzi aliwataka wanufaika wa michango ya benki hiyo kuvitumia vyema vitu vilivyotolewa kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Sophia Kizigo wakati akipokea msaada huo kwa niaba ya wilaya yake aliipongeza benki hiyo kwa ukarimu wake na kuongeza kuwa, “msaada huo umekuja wakati mwafaka kwetu huku tukijitahidi kuboresha mazingira ya kujifunzia mashuleni,”
Kizigo alibainisha kuwa madawati 100 yaliyotolewa na benki katika wilaya yake yatasaidia kwa kiasi kikubwa yatasaidia wanafunzi kujifunza katika mazingira mazuri zaidi na kuyataka wafanyabiashara Na na kampuni nyingine zinazoofanya biashara wilayani humo kuunga mkono juhudi zake za maendeleo.
“Tumefurahi sana kwa mchango huu na ni Imani yetu kuwa sasa wanafunzi wetu hawatabanana tena kama ilivyokuwa. Sasa watastarehe wanapojifunza,” alisema.