NA FARIDA RAMADHANI, DODOMA
WIZARA ya Fedha na Mipango imesema kuwa Serikali imeanza mchakato wa kuandaa Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo (Vision 2050), ambayo itatoa maono na kuweka malengo ya Taifa kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jenifa Omolo, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hafla ya uzinduzi wa Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unaotarajiwa kufanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Philip Mpango, Aprili 3, 2023 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.
Omolo amesema Maandalizi ya Dira mpya ya 2050 yanakidhi matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuisha kwa kipindi cha utekelezaji wa Dira iliyopo sasa ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, inayotarajiwa kumaliza muda wake baada ya miaka miwili ijayo.
“Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 utekelezaji wake utafikia tamati mwaka 2025 ambapo hadi sasa utekelezaji wake umeliwezeshaTaifa kupiga hatua kubwa ya maendeleo katika nyanja mbalimbali hususan za kijamii, kiuchumi na kisiasa”, amesema Omolo.
Amesema kuwa historia ya upangaji wa mipango nchini imeanza kuanzia nchi ilivyopata uhuru ambapo matamanio yalikuwa kupambana na maadui watatu wa Taifa, ukiwemo ujinga, umaskini na maradhi.
“Mwaka 1964, Tanzania ilifanikiwa kuandaa Mpango wa kwanza wa Muda Mrefu wa miaka 15 ambao ndani ya utekelezaji wake uliimarishwa na Azimio la Arusha la mwaka 1967 na Mpango wa Pili wa Muda mrefu uliandaliwa Mwaka 1981 ”, amebainisha Omolo.
Amesema utekelezaji wa mipango hii ulienda sambamba na utekelezaji wa programu mbalimbali zilizosimamiwa na Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa, (IMF) zikiwa na lengo la kuleta utulivu wa kiuchumi na marekebisho ya kimuundo nchini.
“Katika kufanikisha malengo yaliyopangwa, Serikali ilianza mchakato wa maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa (TDV 2025) mwaka 1995 ambao ulikamilika mwaka 2000”, ameeleza Omolo.
Amesema utekelezaji wa Dira hiyo ulianza kupitia programu za kupunguza umaskini kama Mkakati wa Kupunguza Umaskini (PRS I) mwaka 1999/2000 – 2002/03, unaojulikana kama Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA I) mwaka 2004/05 – 2009/10 na MKUKUTA II mwaka 2010/11 -i 2014/15.
Omolo amebainisha kuwa mwaka 2009/10, Serikali ilifanya tathmini ya utekelezaji wa Dira 2025 kupitia mikakati na programu za maendeleo na kubaini kuwa kuna uhitaji wa Taifa kuanza kupanga vibaumbele vya nchi ambapo Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu (LTPP) 2011/12 – 2025/26) uliundwa.