Na Mwandishi Wetu
KATIKA kuadhimisha mwezi mtukufu wa Ramadhan, Benki ya NMB mwishoni mwa wiki iliandaa hafla ya futari kwa wateja wake mkoani Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kuendeleza mahusiano mazuri na wateja wake.
Hafla hiyo ya futari iliwakutanisha zaidi ya watu 350 na kuhuduriwa na Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Bin Zuberi ambaye alitoa wito wa umoja katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna alisema hafla ya futari ni sehemu ya utamaduni wa benki hiyo wa kuenzi na kusherehekea mwezi mtukufu wa Ramadhani.
“Benki yetu ya NMB imekua ikiandaa futari kwa wateja wetu kila mwaka kama ishara ya shukrani kwa kuendelea kuaminiwa na wateja kwa kutufanya kuwa benki ya chaguo lao. Tumeanza na mkoa wa Dar es Salaam leo na tutaendelea kuandaa shughuli kama hii kwa wateja wetu kote nchini ikiwa ni pamoja na Unguja na Pemba katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani,” Zaipuna alisema.
Zaipina aliongeza “Tunapoadhimisha siku za baraka za mwezi huu mtukufu, sisi kama benki tunatumia fursa hii kushiriki pamoja na wateja wetu Waislamu. Matukio kama hili yanatupa fursa kutoa shukrani zetu kwa wateja wetu kwa kuendelea kutuamini.
Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki hiyo Juma Kimori wakati wa hafla hiyo alisisitiza tena dhamira ya benki hiyo kuendelea kutoa bidhaa za kipekee kwa wateja wake.
“Matukio kama hili hutupatia jukwaa muhimu kuelewa mahitaji ya wateja wetu vyema huku tukiimarisha uhusiano wetu. Kama benki, tutaendelea kutoa bidhaa za kipekee zinazokidhi mahitaji ya wateja wetu, “Kimori alisema.
Naye Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Bin Zuberi wakati wa hafla hiyo aliipongeza Benki ya NMB kwa kuandaa hafla hiyo ya futari na kuongeza kuwa jumuiya ya Kiislamu inajisikia kuthaminiwa, kutambuliwa na kuheshimiwa.
“Benki ya NMB na uongozi wake wameonyesha upendo kwa jamii ya waislamu. Mwaliko wa kwanza wa futari nilioupata mwaka huu ni kutoka Benki ya NMB na cha kushangaza mwezi mtukufu wa Ramadhani ulikuwa bado miezi kadhaa. Nimefurahi kwamba hatimaye tumefika katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na tumekutana kwa ajili ya tukio hili la futari,” Sheikh Zuberi alisema.
Sheikh Zuberi katika hafla hiyo aliwataka waislamu na wasiokuwa waislamu kutenda mema hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.
“Kuna haja ya kuhakikisha kwamba tunaimarisha maadili yetu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Katika miaka ya hivi karibuni, tumeshuhudia kuporomoka kwa maadili si tu nchini Tanzania bali Afrika kwa ujumla,” Sheikh Zuberi alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saadi Ahmed wakati wa hafla hiyo aliipongeza benki hiyo kwa kuendelea kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wa Dar es Salaam.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wakuu wa serikali wakiwemo Wakuu wa Wilaya kutoka mkoa wa Dar es Salaam na Meya wa Dar es Salaam Omar Kumbi la Moto pamoja na wengine.