*Sasa vyeti vyote kuwa na saini moja ya Mtendaji Mkuu
Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
KWA muda mrefu Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) imekuwa na dhamana katika utoaji wa habari nzuri na thabiti juu ya matukio muhimu maishani, uunganishaji wadhamini, utunzaji wa mali chini ya udhamini za mtu aliyefariki, muflisi, na watoto walio chini ya umri wa utu uzima ili kuwezesha sheria kuchukua mkondo wake.
RITA ilizinduliwa rasmi tarehe 23 Juni 2006 na inachukua nafasi ya ile iliyoitwa Idara ya kabidhi Wasii Mkuu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali, Wizara ya Katiba na Sheria. Ni Wakala chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu katika Wizara ya Katiba na Sheria.
Historia ya RITA inaanzia nyuma mnamo mwaka 1917 wakati serikali ya kikoloni ya Ujerumani ilipotunga sheria ya usajili wa vizazi na vifo (Tangazo Na. 15 ya 1917 (Eneo la wananchi). Wakati Waingereza walipoichukua Tanganyika (Tanzania Bara) kutoka kwa Wajerumani waliutambua utaratibu wa usajili wa vizazi na vifo uliowekwa kwa sheria za Kijerumani kwa kutambua daftari chini ya Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo, 1920 (sura ya 108).
Ikumbukwe kwamba chini ya mataifa yote mawili ya kikoloni usajili wa vizazi na vifo haukuwa wa lazima kwa Waafrika.
Kati ya mwaka 1920 na 1960 serikali ya kikoloni ya Kiingereza ilikuja na sheria zaidi kuhusu matukio muhimu ya kimaisha na masuala mengine. Sheria hizi ama zilisimamiwa kwa ujumla au kwa sehemu yake na ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu/Msajili Mkuu.
Kutokana na hali hiyo RITA imekua ikifanya mageuzi kadhaa ikiwamo mfumo mpya wa eRITA, ambao unakuwezesha kutuma maombi ya huduma za Vizazi, Vifo, Ndoa na Udhamini kwa njia ya kidigitali popote ulipo.
eRITA ni rahisi kutumia, salama na itakuwezesha kupata huduma kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu.
Mtendaji Mkuu wa RITA, Angela Anatory, hivi karibuni alikutana na Wahariri katika mkutano wa mwaka uliofanyika mjini Morogoro, ambapo anasema mfumo mpya sasa utakuwa ni rahisi kwa kila mtanzania ambaye kwa muda mrefu amekuwa amekuwa akitembea umbali mrefu kufuata huduma za usajili pamoja na kutumia siku nzima kusubiri kuwasilisha fomu au cheti.
“Haya kwetu ni mageuzi makubwa sasa tunakwenda kuwafanya Watanzania wawe na uwezo wa kujaza fomu kwa njia ya mtandao ikiwamo kuingiza taarifa za mtoto, cheti cha kifo au ndoa na mtu atakuwa na uwezo wa kujaza wapi angependa akipate cheti chake.
“Mfumo huu wa utabebwa kwenye huduma 34 katika dirisha moja lakini kwa sasa zinapatikana huduma 12 na kadri ya siku zinavyokwenda tutakuwa tunapakia huduma kwenye tovuti yetu ya RITA. Kupitia eRITA mtu atakuwa na uwezo wa kujaza fomu ambayo itapokea usajili mpya, kubadili cheti cha kuzaliwa na uhakiki wa cheti cha kuzaliwa.
“…pia mwananchi atakuwa na uwezo wa kutuma maombi ya usajili mpya wa cheti cha kifo, kubadili cheti cha zamani na uhakiki wa cheti cha kifo. Jambo ambalo tunapenda Watanzania waelewe vyeti vyote kwa sasa vitakuwa na saini moja ya Mtendaji Mkuu wa RITA lengo likiwa ni kudhibiti vyeti na wtu kuingilia mifumo yetu kinyume cha utaratibu,” anasema Angela
Licha ya hali hiyo Angela anasema kuwa pia mfumo huo utawawezesha watu kuomba leseni za kufungisha ndoa, kuhuisha leseni ya zamani, kusajili ndoa zilizofungwa nje ya nchi, shahada ya kutokuwepo pingamizi na kununua vyeti vya ndoa kwa wafungishaji.
“Pia eRITA itawafanya wanadhamini kutuma maombi yao ya kusajili Bodi ya Wadhamini, marejesho ya wadhamini, taarifa ya kubadili anuani ya Posta, taarifa ya kubadili dhamana au Katiba, kupata kibali cha kimiliki ardhi na upekuzi wa taarifa za wadhamini. Huduma zote hizi tumeona tuzilete kwenye mfumo wa kidigitali na mtu anaweza kufanya popote alipo Tanzania ili mradi awe na simu janja,” anasema
Anasema ili mwananchi aweze kutumia huduma hiyo anapaswa kuingia kwenye tovuti ya www.rita.go.tz na baada ya kuingia atatakiwa kubofya kitufe kulichoandikwa eRITA muhimu kama ulishajisajili na kuwa na akaunti itakupeleka kwenye kwenye page na kuweka nywila yake (neno la siri) na baada ya hapo utatumia ujumbe kwenye barua pepe na kufungua ujumbe wako.
Mtendaji Mkuu huyo wa RITA, anasema ni lazima jamii ikubali mabadiliko hayo chanya jambo ambalo itsaidia kuondoa msongamano wa watu katika ofisi za RITA zilizopo katika wilaya mbalimbali nchini.
“Narudia tena hapa kufafanua kwamba mfumu huu utamuwezesha mwananchi kuweza kujaza taarifa zake ikiwamo yeye mwenyewe atasema wapi angependa akachukue cheti chake hata ikiwa katika ofisi ya Kata au Kijiji kitamfuata huko badala ya yeye kutembelea umbali mrefu kufuata huduma zetu kwenye ngazi za wilaya,” anasema Angela
Anasema dhima ya RITA ni kusimamia haki kwa usimamizi wenye ufanisi wa kumbukumbu muhimu za maisha ya binadamu, ufilisi na udhamini ili kuchangia katika Maendeleo ya Taifa.