Na MWANDISHI WETU
-DODOMA
Katika bajeti ya 2022/23, Serikali imetoa ruzuku ya Sh bilioni 17 kwa vyama sita vya siasa vyenye sifa za kupewa ruzuku.
Vyama hivyo ni CCM, Chadema, NCCR- Mageuzi, ACT Wazalendo DP na CUF na kwamba itaemdelea kufanya hivyo ikiwa ni takwa la kisheria.
Hayo yamesemwa leo Aprili 5, 2023 Bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akisoma hotuba ya Makadilio ya Mapato na matumizi kwa ofisi na wizara zilizo chini yake.
Kutolewa kwa kauli hiyo ni dhahiri inakwenda kuzima minong’ono ya muda mrefu kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), hakijachukua ruzuku ya Serikali tangu ulipomalizika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Hatua hiyo imekuwa ikiibua mijadala mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii na vijiweni juu ya Chadema ambao viongozi wake wamekaririwa mara kadhaa wakidai kwamba hawatachukua ruzuku ya Serikali ingawa tangu yalipomalizika maridhiano ya kitaifa yaliyosimamiwa na mkuu wa nchi Rais Samia Suluhu Hassan.
Ingawa katika hotuba yake ya bajeti Waziri Mkuu Majaliwa, hakusema vyama hivyo kila kimoja kimechukua kiasi gani cha fedha kwa wakati huu.
Kutokana na hali hiyo Majaliwa, amesema demokrasia imeendelea kuimarika nchini ikiwemo uhuru wa vyama vya Siasa na nyombo vya habari katika kujenga nchi yao.