Na MWANDISHI WETU
-DODOMA
Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda ameiomba Serikali kuliangalia suala la vitambulisho vya Taifa kwani watanzania wengi bado hawajavipata.
Akichangia bungeni mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2023-2024, leo Aprili 6,2023 Mbunge huyo amesema Serikali inakwamisha maendeleo ya watu kwa kushindwa kuwapatia vitambulisho vya Taifa.
Amesema wapo wanaotaka kuingiza umeme,maji na kuomba pasipoti lakini wanakwama kwa sababu ya kukosa vitambulisho vya Nida
“Na hili ningekuomba sana kwa sababu nimelisema katika ofisi ya Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri Mkuu ndio msimamizi mkuu wa Serikali tunakujua wewe ni mtu makini sana.
“Kama hapa kati kati ulitikisika ni vinenoneno vya wapambe usijali simama imara fanya kazi umeaminiwa, sisi katika nchi hii ni historia Waziri Mkuu mmoja kuaminiwa na Marais, chapa kazi hakuna kurudi nyuma, simamia serikali,” amesema Mbunge huyo.
Pia, mbunge huyo amesema kuna haja ya Serikali kuangalia namna bora ya kuwasaidia wasafiri wanaolala katika standi mbalimbali nchini.
“Mimi naishauri Serikali wekeni utaratibu wa kisaulama mabasi ya Kigoma yaondoke usiku Dar es salaam, yapite maeneo yote mchana sio watu waje kulala Stand ya Magufuli au Kaliua kadri tunavyowachelewesha ndivyo shughuli za uzalishaji zinazidi kuchelewa,”amesema Mbunge huyo