Na MWANDISHI WETU
-DODOMA
Waziri wa Fedha na Mipango,Dk. Mwigulu Nchemba amesema mifumo ya malipo ipo imara huku akidai waliohusika kuongeza fedha za manunuzi ya ndege hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.
Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo leo bungeni jijini Dodoma, wakati akimpa taarifa Mbunge wa Viti Maalum, Ester Matiko (Chadema), alipokuwa akichangia bungeni mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2023-2024.
Katika mchango wake Matiko amedai kuna ubadhirifu mkubwa katika ununuzi wa ndege huku wahusika wakikaa kimya bila kusema jambo lolote.
Kauli hiyo ya Waziri Mwigulu inakuja siku chache tangu Rais Samia Suluhu Hassan, kuonyesha wazi kuchukizwa kwake na ongezeko hilo la fedha za manunuzi ya ndege mpya ya mizigo kinyume na fedha ambazo zilizokuwa kwenye mkataba wa awali akataka Watumishi wa Serikali waliokubali ongezeko hilo bila kuhoji waachie nafasi zao kwakuwa hawana uchungu na fedha za Watanzania.
“Kuna mradi hapa tumetengeneza Ndege ya mizigo ambayo tunakaribia kuipokea, last Installments ilikuwa tulipe Dola milioni 37, invoice imekuja dola milioni 86….. unauliza mkataba ulisemaje? hii imetokana na wapi?, ooh vifaa vimepanda bei, vipi? mkataba wetu ulisemaje”
Kutokana na hali hiyo Mbunge Matiko, amesema haikubaliki na haiingia akilini kwani litakuwaTaifa la ajabu kuruhusu watendaji hao kuendelea kukaa huku akimtupia kijembe Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba, kwamba kila siku anavaa tai ya Tanzania inaoonyesha uzalendo laini akahoji uko wapi uzalendo huo.
Katika taarifa yake Dk. Mwigulu amesema utaratibu wa malipo uliowekwa hapa nchini ni imara hauna vitu vya ovyo ovyo vinaweza kupita.
Amesema hakuna malipo ya kila mwezi yanayoenda kufanyika bila Rais kujua na mahitaji yote yalikienda Wizara ya Fedha na Mipango wanaombea ridhaa kwa Rais.
“Na hata hilo la ndege unalolisema yalipoletwa mahitaji Wizara ya Fedha tuliliona linaongezeko ambalo kama ni la kimkataba lazima tupate ushauri wa Mwanasheria Mkuu,”amesema Waziri Mwigulu.
Alipoulizwa na Spika kama anaipokea taarifa hiyo, Matiko alisema: “Mheshimiwa Spika nitakuwa sijitendei haki, siipokei.” Mheshimiwa Spika
Akiendelea kuchangia Mbunge huyo amehoji malipo hayo ni makubwa je yale madogo ambayo yamekuwa yakifanywa na watendaji wa Serikali inakuwaje.