Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
Chama cha ACT Wazalendo, kimefanya uchambuzi wa hotiba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu Mapitio ya kazi na mwelekeo wa Serikali na makadirio ya matumizi ya bajeti kwa Mwaka wa Fedha wa 2023/2024 wa Ofisi ya Waziri Mkuu wizara na taasisi zake na kushauri masualaa kadhaa ikiwamo suala la hali ngumu ya maisha na ajira kwa vijana.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kivuli ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Dorothy Semu amesema kuwa Aprili 5, 2023 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa , aliwasilisha Bungeni mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa Fedha wa 2022/2023 jijini Dodoma.
Amesema katika kuendeleza wajibu wa kuisimamia Serikali, ambaye yeye ndiye Msemaji Mkuu wa Kamati ya Kuisimamia Serikali ya ACT Wazalendo (Waziri Mkuu Kivuli) alitoa maoni yake kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu aliyeitoa Bungeni.
Amesema kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu Waziri Mkuu ndiye msimamizi wa shughuli za kila siku za Serikali. Kwa hiyo ni matarajio ya wengi kuwa hotuba yake ingekuja na mwelekeo na majawabu ambayo yangesaidia kutatua changamoto mbalimbali ambazo nchi yetu inakabiliana nazo kwa sasa zikiwemo changamoto za hali ya kiuchumi, mwenendo wa kisiasa na hali ya usalama.
“Hivyo basi kutokana na uchambuzi wetu, tumeona yapo masuala makubwa saba yanayohusu maisha ya watu ya kila siku hayajaguswa kwa kupatiwa ufumbuzi. Hali ngumu ya maisha suala la hali ya maisha ya wananchi (hususani mfumuko wa bei na kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu) bado Serikali haijaweka mkazo kujiandaa kukabiliana na mwenendo huu kiasi cha kutoa nafuu kwa wananchi.
“Hotuba ya Waziri Mkuu inataja takwimu za kitaalamu (ambazo hazigusi uhalisia) kuonyesha kama hali ni nzuri. Hofu yetu ni kuwa mwelekeo huu wa Serikali unaweza kupelekea kipindi kijacho tena kuwa kwenye hali ngumu zaidi kwakuwa hakuna hatua madhubuti za kutoa nafuu kwa wananchi.
“ACT Wazalendo tunaielekeza Serikali kununua na kuhifadhi chakula cha kutosha angalau miezi 3 kutokana na chakula kitachovunwa mwaka huu ili kujilinda na upungufu wa chakula. Kutokana na ukweli kuwa kwa maeneo mengi nchini uzalishaji unaweza kuwa sio mzuri kwa mwaka huu.
“Hatua hii itawezakana kwa Serikali kujenga uwezo wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa kutenga bajeti ya kutosha ya kununua chakula (Tani Milioni 1.5 za Mahindi, Tani laki 5 za Mpunga, Maharagwe tani Milioni 1). Aidha, kuwezeshwa Bodi ya mazao mchanganyiko kununua na kusambaza chakula kwenye eneo linaloonyesha uhaba/upungufu wa chakula.
“Suala la hali ya ukosefu wa ajira na maslahi ya wafanyakazi nchini. Ofisi ya Waziri Mkuu inahusika moja kwa moja na masuala ya ajira na uwezeshaji kupitia Wizara ya Vijana, kazi na ajira. Mwenendo na hali ya ukosefu wa ajira nchini inazidi kuwa tata sana, uchumi wetu unazidi kupunguza uwezekano wa kuzalishaji ajira zenye staha na shughuli za kueleweka za kuwapatia vijana vipato ili kumudu maisha yao.
Pia amesema kuwa suala la kuhamishwa kwa wananchi (jamii ya wafugaji) Ngorongoro bado hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ameleza kuwa mchakato wa kuwahamisha kwa hiyari wananchi wa jamiii ya wafugaji katika hifadhi ya Ngorongoro limefanyika kwa kuzingatia haki za wanaohama.
“Waziri Mkuu anasema katika hotuba yake ukurasa wa 39 anasema” zoezi hilo limefanyika kwa umakini mkubwa na kwa kuzingatia haki za wanaohama. Hadi kufikia Januari, 2023 jumla ya kaya 1,524 zenye watu 8,715 na mifugo 32,842 zilikuwa zimejiandikisha kwa ajili ya kuhama kwa hiari kwenda Kijiji cha Msomera. Kati ya kaya hizo, kaya 551 zenye39 watu 3,010 na mifugo 15,521 tayari zimehamishwa kwa hiari kwenda Msomera,” amesema Semu