NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Bima Tanzania (TIRA), imeitaja huduma mpya na ya kipekee ya Bima ya Kontena (Container Insurance Scheme) iliyoingizwa sokoni na Benki ya NMB kwa kushirikiana na Kampuni ya Strategis Insurance, kuwa ni suluhu ya changamoto katika Sekta ya Usafirishaji, ambayo ni miongoni mwa nguzo muhimu za kukuza na kujenga uchumi imara wa taifa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa TIRA, Abubakar Ndwata, alipomwakilisha Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Dk. Saqware Baghayo, wakati wa uzinduzi WA huduma hiyo jijini Dar es Salaam, ikilenga kutanua wigo wa upatikanaji wa bima kwa wadau wa sekta hiyo na kuwapunguzia gharama za usafirishaji.
Awali akimkaribisha Ndwata, Mkuu wa Idara ya Bima wa NMB, Martine Massawe, alisema Bima ya Kontena italeta uhakika usalama wa kontena, sanjari na kuondoa ulazima kwa wasafirishaji kuweka fedha ya dhamana (deposit) kwa kila kontena au kulipa gharama za uharibifu wa kontena.
Massawe alibainisha kuwa, NMB inajisikia fahari kufanikisha uzinduzi huo wa kihistoria, unaoenda kuacha alama kubwa katika Sekta ya Usafirishaji nchini na kuwaondolea wadau wake gharama za malipo yatokanayo na ucheleweshaji wa kurejesha kontena, pamoja na uharibifu wa mali utakaosababishwa na kontena (third party damages).
“NMB tumekuwa vinara wa jitihada za kila mara na kila namna za kuzifikia sekta mbalimbali (zikiwemo za kimkakati) kwa namna moja ama nyingine ili sisi tuwe chachu ya kuzitatua changamoto zinazotesa wadau wa sekta hizo na kukwamisha harakatk zao za kukua kiuchumi na kuchangia pato la Taifa.
“Kwa kuzitambua changamoto hizo, na nia ya dhati ya kusaidia kupambana nazo, NMB ikaona ni vema kushirikiana na Strategis Insurance, tukaja na bima hii ya kontena, ambayo ni mahsusi kwa kampuni, mashirika, taasisi na mtu binafsi anayesafirisha mizigo katika kontena za futi 10, 20 na 40,” alisisitiza Massawe.
Akiizungumzia huduma hiyo mpya, Ndwata alisema kwamba Bima ya Kontena ni ‘product’ inayoakisi ubunifu wa mkubwa uliofanywa na Strategis Insurance na NMB, ambayo itakuwa chachu ya kusapofj jitihada za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambazo zimeipaisha Tanzania na kushika nafasi ya sita ya ukubwa kiuchumi barani Afrika.
“Madhumuni ya bidhaa ni kuamsha mchango wa Sekta ya Bima kiuchumi, ambao kwa sasa uko chini. Kama tulivyoona majuzi, takwimu zimeitaja Tanzania kuwa ya sita kwa ukubwa wa ukuaji kiuchumi Afrika, na hii ni kutokana na juhudi za Rais wetu.
“Maana yake ni kuwa kuna ongezeko kubwa la ‘middle class’ na wakata bima. Kwahiyo ukuaji huo ni fursa kwa tasnia ya bima kuja na bunifu kama hizi ili kuongeza mchango wetu katika ukubwa wa uchumi wetu,” alisema Ndwata huku akieleza kuwa mamlaka yake imejipanga vya kutosha kuweka mazingira wezeshi ya utoaji huduma za bima chino kwa Rashidi, kampuni na mashirika mbalimbali.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya Strategis Insurance, Dk. Flora Minja, alibainisha kwamba, Ripoti za Kiuchumi kutoka kwa wachumi zinaonesha kwamba inakua kwa kasi, na walipozifanyia tathmini wakagundua pengo katika Sekta ya Usafirishaji, ndipo wakaja na wazo lililozaa Bima ya Kontena na kuipongeza TIRA kwa kuiidhinisha.
“Hii ni huduma mpya na ya kipekee kabisa nchini Tanzania, ambayo inakuja kuwa suluhu ya majanga mbalimbali katika sekta ya usafirisha, yakiwemo ya upotevu, wizi na hasara nyingine kama hizo zinazokwamisha ustawi biashara na uchumi wa msafirishaji mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,” alisema.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Strategis Insurance – Divisheni ya Huduma Zisizo za Afya, Jabir Kigoda, alisema sababu kubwa zilizounganisha kampuni yake na NMB ni ukubwa wao katika tasnia zao, wanaoamini utakuwa chachu ya ufanisi kwa kuzingatia ukweli kuwa wao wako ndani ya kampuni tatu bora za bima Tanzania, huku NMB ikiwa kinara miongoni mwa taasisi za fedha.