Na Mwandishi Wetu
-Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuheshimu na kuthamini haki ya uhuru wa habari na kujieleza.
Hayo ameyasema Mei 3, 2023 Jijini Zanzibar katika maadhimisho ya uhuru wa habari ambayo yamehudhuriwa na wanahabari wenyewe pamoja na mabalozi wa nchi mbalimbali.
Dk. Mwinyi, amesema kuwa katika maeneo mbalimbali nchini, kumekuwa na ongezeko kubwa la uanzishwaji wa vyombo vya habari huku akisisitiza kuanzishwa kwa vyombo hivyo kunatokana na mazingira bora yaliowekwa na Serikali zote mbili.
Kutokana na hali hiyo ametolea mfano na kusema kuwa kwa mujibu wa takwimu hadi sasa, Tanzania ina idadi ya magazeti yaliosajiliwa ni 312 huku kukiwa na idadi kubwa ya vyombo vya habari vya mtandaoni.
“Baada ya Tanzania kupata uhuru kila mmoja ni shahidi kuwa tulikuwa na magazeti 10 pekee ambayo ndio yalikuwa yakifanya kazi hapa nchini,’’ amesisitiza.
Akizungumzia kuhusu kupatikana kwa sheria mpya ya habari Zanzibar, amesema tayari Serikali imefikia hatua nzuri na kwa sasa tayari muswada wa sheria hiyo umeshakamilika na wanasubiri kuwasilishwa kwenye Baraza la Wawakilishi.