Na Mwandishi Wetu
-Dar es Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, CPA Amos Makalla ameelekeza Jukwaa la Uwekezaji Wanawake Kiuchumi Mkoa huo kuja na mpango kazi wa kuleta mabadiliko chanya kwa Wanawake ikiwa ni pamoja na kuwafikia wengi zaidi ili kuleta tija na mabadiliko ya kiuchumi.
RC Makalla ametoa maelekezo hayo leo Mei3, 2023 wakati ufunguzi wa Mafunzo maalumu kwa viongozi wa majukwaa ya Wanawake mkoani humo ambapo ameelekeza mafunzo waliyopata wakayashushe ngazi ya wilaya, kata na mitaa ili kunufaisha wanawake wengi zaidi.
Aidha Makalla ameelekeza dhana ya uwezeshaji wanawake kiuchumi iende sambamba na kuwapatia fursa mbalimbali zinazopatikana ili kuwakwamua kiuchumi.
Pamoja na hayo RC Makalla amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alilotoa kwa kila mkoa kuyalea na kuyatunza majukwaa ya wanawake.
Sanjari na hayo, CPA Makalla amewataka viongozi wa majukwaa ya wanawake kuelimisha wanawake kuhusu umuhimu wa kufanya mambo machache kwa ufanisi na tija na sio kujaribu kila biashara.