NA ANDREW CHALE,
DAR ES SALAAM.
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wake, Felista Mauya kimetoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kufuatia kutoa agizo lake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuitisha kikao maalum cha Baraza la Vyama vya siasa kutathimini mapendekezo ya kikosi kazi.
Katika taarifa hiyo, Rais ametoa agizo hilo kwa Jaji Mutungi, kuitisha kikao hicho kwa lengo la kuwashirikisha wadau kutathimini utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi kilichokuwa kikiratibu maoni ya wadau kuhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa hapa nchini.
Agizo hilo alilitoa siku ya tarehe 06 Mei, 2023 wakati wa kikao na viongozi mbalimbali wa serikali kilichofanyika Ikulu Chamwino.
Kwa vipindi mbalimbali, kumekuwa na changamoto ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume na vikosi mbalimbali vilivyoundwa kuhusu utatuzi wa changamoto za demokrasia nchini. Hivyo, hatua hii ya kufanya tathimini ya utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi ni hatua yenye kuleta tija na mwanga wa utekelezaji wa mapendekezo hayo.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunatoa wito kwa kikao hicho kinachotarajiwa, kuja na utaratibu thabiti na endelevu wa namna ya kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi cha Demokrasia ya Vyama Vingi kwa uwazi na ushirikishwaji mpana wa jamii.