NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
KATIKA kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuharakisha maendeleo ya kiuchumi, Benki ya NMB na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU), ambayo yamepongezwa na SMZ, iliyokiri kuwa taasisi hiyo kinara ya fedha nchini ni mbia bora na sahihi katika kuhimili vita ya ushindani kwenye Sekta ya Uwekezaji Afrika.
Makubaliano hayo yamesainiwa Zanzibar Mei 9, yakilenga kuendeleza ushirikiano katika kutengeneza mifumo ya kufuatilia taarifa na kuwadumia wawekezaji visiwani hapa, sanjari na kutangaza vivutio vya uwekezaji nchini, pamoja na NMB kutoa suluhishi za kifedha na ukusanyaji wa mapato kwa njia za kidijitali kwa wawekezaji.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa SMZ, Mudrik Ramadhani Soraga, alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo, akishuhudia utiaji saini huo uliofanywa na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa NMB, Ruth Zaipuna na Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA, Sharif Sharif, mbele ya Dkt. Khatibu Mwadini, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Soraga aliishukuru na kuipongeza NMB kwa aina ya ushirikiano inaotoa kwa Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar inayoongozwa na Rais, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ikiwemo udau katika kukuza Uchumi wa Buluu na sasa kuipa nguvu za kuhimili ushindani katika Uwekezaji, pamoja na kusapoti mabadiliko ya kiutendaji kwa njia ya kidigitali ya Serikali na taasisi zake.
“Aina ya ushirikiano wa NMB kwa Serikali ya Awamu ya Nane Zanzibar ni wa kuigwa, ikiunga mkono kila jitihada za kutoa huduma bora na kukuza ufanisi katika kuvutia wawekezaji na nikiri kwamba isingekuwa rahisi kwa SMZ na taasisi zake kupata mbia bora na sahihi zaidi ya NMB.
“Usipofanya ukuzaji huwezi kushindana na usiposhindana huwezi kukuza uwekezaji. NMB imetupa nguvu hiyo, ikiwezesha watendaji wa taasisi Serikali kwenda nje ya nchi kujifunza namna ya kukuza ufanisi katika uwekezaji,” alisema Waziri Soraga.
Awali, Zaipuna aliishukuru ZIPA na SMZ kwa kuikaribisha NMB kuwa mshirika wa karibu katika safari ya kuiletea Zanzibar maendeleo chanya ya kiuchumi na kijamii na kusisitiza ya kwamba benki yake inatambua na kuheshimu nia ya dhati ya Serikali kupitia ZIPA, ya kuishirikisha taasisi yake katika utekelezaji wa mipango ya kuwahudumia wawekezaji kwa ufanisi zaidi.
Alifafanua ya kuwa, Machi mwaka huu, SMZ kupitia ZIPA, ilizindua muongozo wa uwekezaji Zanzibar na mfumo wa kielektroniki wa kuhudumia wawekezaji, ambapo kupitia mfumo huo, Wawekezaji waliweza kujisajili, kufanya maombi ya cheti cha uwekezaji, mpaka kupata cheti cha uthibitisho wa uwekezaji wao.
“Hivyo basi, leo tunasaini rasmi makubaliano ya miaka mitatu ya ushirkiano kati ya NMB na ZIPA, ambayo yanalenga kuendelea kushirikiana katika kutengeneza mifumo ya kufuatilia taarifa na kuwadumia wawekezaji hapa Zanzibar.
“Kipekee hapa ni utekelezaji wa mfumo kwa awamu ya pili ambapo pamoja na mambo mengine, utamwezesha mwekezaji kuhuisha cheti ambacho kitakuwa kimeisha muda wake. Awamu hii ya pili pia itaweza kuunganisha mfumo wa ZIPA na ile ya Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato na Wakala wa Usajili Mali na Biashara (BPRA),” alibainisha.
Zaipuna aliyataja malengo mengine ya makubaliano hayo kuwa ni pamoja kuendeleza mashirikiano katika kutangaza vivutio vya uwekezaji nchini, sambamba na NMB kutoa suluhishi za kifedha na ukusanyaji wa mapato kwa njia za kidijitali kwa wawekezaji.
“NMB tunakaribisha wawekezaji kushirikiana nasi katika uwekezaji wao hapa Zanzibar, kwani benki ina uwezo, nia, uzoefu na utayari mkubwa katika kuleta masuluhisho mbalimbali yanayoakisi uwezo wetu wa kidigitali na kuzingatia mahitaji halisi ya makundi mbalimbali ya wawekezaji,” alisisitiza.
Alizitaja sababu kubwa za wawekezaji kuitumia benki yake kuwa ni pamoja na mtaji mkubwa wa NMB ambao ni zaidi ya Sh. Trilioni 1.6, kiwango cha juu cha mkopo kwa mteja mmoja (single Borrower Limit) zaidi ya bilioni 350, pamoja na idadi kubwa ya wateja ambapo NMB ina akaunti za wateja zipatazo milioni 6.
Kwa upande wake, Shariffa alisema ZIPA inayo kila sababu ya kujivunia kutamatika kwa mazungumzo chanya ya muda mrefu yanayoakisi dhamira ya dhati ya NMB katika kuinyanyua Sekta ya Uwekezaji na kuunga mkono malengo ya taasisi yake chini ya mwamvuli wa Huduma Bora kwa Wawekezaji.
Alibainisha kuwa ni matumaini yao kwambaushirikiano wao NMB utaongeza kasi ya utoaji huduma bora na rafiki kwa wawekezaji wote visiwani Zanzibar, ambao ndilo lengo la Makubaliano yao ya takribani mwaka mzima yaliyofanikisha utiaji saini huo,
“Makubaliano haya ambayo yatazinduliwa na Rais, Dk. Hussein Mwinyi wakati wa sherehe zijazo za Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar, yana maana kubwa kwetu sote, yakienda kuboresha kasi ya utoaji huduma kwa wawekezaji kwa kuutumia mifumo ya kielektroniki ya kisasa.
“Ni Makubaliano yatakayojikita katika maeneo mbalimbali, yakiwemo ya kuandaa mifumo ya ukusanyaji taarifa, kuboresha mifumo ya uwekezaji, kubadilishana taarifa na kutoa mikopo kwa wawekezaji,” alibainisha Sharif.
Kwa nyakati tofauti, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Serikali Mtandao (e GAZ), Said Said na Mkurugenzi Mkuu wa Mkongo wa Mawasiliano (ZICTIA), Shukuru Awadhi Suleiman, waliyapongeza makubaliano yaliyosainiwa baina ya NMB na ZIPA, ambayo yanaenda kuwa chachu ya ukuzaji sekta ya uwekezaji Zanzibar.