Na Mwandishi Wetu
RAIS Mstaafu Jakaya Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education) – GPE) yuko Seoul, Korea Kusini kwa ajili ya kukutana na viongozi wa Serikali na mashirika mbalimbali ya Korea Kusini.
Lengo ni kwa ajili ya kujadili mikakati ya kuendelea kuboresha elimu katika nchi zinazoendelea. GPE ambayo ilianzishwa na nchi za G7 miaka 20 iliyopita, imeendelea kupigania elimu kwa ajili ya mtoto wa kike na wa kiume kwa kuomba kuungwa mkono na nchi na taasisi zinazoweza kuchangia katika elimu duniani.
Kikwete ameambatana na Charles Noth, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo yenye makazi yake Washington DC, Marekani na akiwa Seoul, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Park Yongmin, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini.
Aidha, amekutana na Kaimu Rais wa Shirika la Serikali ya Korea la Maendeleo Kimataifa (KOICA) Lee Yunyoung. Pia amekutana na Mheshimiwa Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mstaafu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Ban Ki-moon.
Kesho Rais Kikwete anatarajiwa kuzungumza na Wabunge wa Korea Kusini na kufanya mazungumzo na Ju-ho Lee ambaye ni Naibu Waziri Mkuu wa Korea Kusini ambaye pia ni Waziri wa Elimu wa nchi hiyo.
Pia ametembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jijini Seoul, Korea Kusini na kuzungumza na wafanyakazi. Akiwa na mwenyeji wake Balozi Togolani Mavura, amewahimiza kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na kuunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.