Na Mwandishi Wetu, Best Media
KATIKA kuendeleza mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi/ Ukimwi, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela ametoa wito kwa wafanyabiashara wa mkoa huo na Watanzania kwa ujumla kuchangia fedha katika Kampeni ya GGML Kili Challenge ainayolenga kukusanya fedha kwa ajili ya kutunisha mfuko wa udhamini wa kudhibiti Ukimwi (ATF) pamoja na taasisi binafsi zinazojihusisha kudhibiti janga hilo.
Mongela ametoa wito huo Mei 14, mwaka huu jijini Arusha katika harambee ya kuchangia Kampeni ya Kili challenge 2023 ambayo inaratibiwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS).
Amesema kampeni hiyo iliyoasisiwa na GGML mwaka 2002, imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za Serikali kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi.
“Fedha hizi zitasaidia wenye uhitaji na baadhi ya fedha zinazopatikana zitawekwa kwenye Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (ATF) kwa ajili ya mwitikio wa UKIMWI nchini,” amesema.
Aidha, Makamu Rais wa Anglo Gold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo amesema kampeni hiyo mwaka huu inatarajiwa kukusanya dola za Marekani milioni moja sawa na Sh bilioni 2.3.
“Fedha hizo ambazo hukusanywa kila mwaka, hulenga kuchangia juhudi za serikali ya Tanzania katika jitihada zake kufikia malengo ya sifuri tatu yaani kupunguza kabisa kwa kufikia asilimia sifuri ya maambukizi mapya, sifuri ya unyanyapaa pamoja na sifuri katika vifo vitokanavyo na UKIMWI,” amesema na kuongeza kuwa;
“GGML imepokea msaada ambao uliiwezesha Kili Challenge kupiga hatua kubwa hadi kufikia kuwa mfuko wa kimataifa, wenye kushirikisha wapanda mlima na waendesha baiskeli kutoka mabara yote na zaidi ya nchi 20.
Amesema mwaka huu wamekuja tena kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, hivyo GGM kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS) tunawakaribisha sana wadau wetu na makampuni mbalimbali kuchangia na kushiriki kampeni hii.
Kurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dk. Leonard Maboko naye ametoa wito kwa Watanzania kuungana na serikali katika kutunisha fedha za mfuko huo wa ATF ihasa ikizingatiwa utegemezi kutoka kwa wahisani katika kipindi cha karibuni umepungua kwa kiasi kikubwa.