Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha zaidi ya shilingi Trilioni 3.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege, reli, meli, vivuko, majengo ya Serikali na ununuzi wa ndege.
Fedha hizo zimeombwa ili kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji kote nchini na hivyo kuimarisha ukuaji wa uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema pamoja na mambo mengine fedha hizo zinatarajiwa kujenga miradi ya kihistoria yenye urefu wa kilometa 2,035 nchini ikiwemo barabara za Kidatu – Ifakara – Lupilo – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Londo – Lumecha hadi Songea KM 435.
Miradi mingine ni barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti River – Lalago – Maswa hadi simiyu KM 339 na barabara ya Handeni – Kibirashi – Kijungu – Kibaya – Njoro – Olboroti – Mrijochini – Dalai – Chambalo – Chemba – Kwa mtoro hadi Singida KM 460.
Aidha, Prof. Mbarawa amefafanua kuwa Serikali itaendeleza ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam – Mwanza KM 1,219 katika vipande vitano vya awamu ya kwanza ya ujenzi ili kuhakikisha vinakamilika kwa wakati na kwa thamani halisi ya fedha.
“Mheshimiwa Spika vipande hivyo ni Dar es Salaam – Morogoro KM 300, Morogoro – Makutupora KM 422, Mwanza – Isaka KM 341, Makutupora – Tabora KM 368 na Tabora – Isaka KM 165 ambavyo ujenzi wake uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, Serikali itaendelea na awamu ya pili ya ujenzi wa SGR sehemu ya Tabora – Kigoma KM 506 ambapo mkataba wake umesainiwa na kwa sasa mkandarasi anakamilisha maandalizi ya ujenzi.
Awali akitaja vipaumbele vya Sekta ya Ujenzi Prof. Mbarawa amesema ni pamoja na kuanza ujenzi wa barabara ya Express way kutoka Kibaha-Chalinze-Morogoro yenye urefu wa KM 205 kwa mfumo wa PPP na kuendeleza ujenzi wa barabara kuu zenye urefu wa KM 350 ambapo kilometa 282 zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na kilometa 68 ni miradi mipya.
“Wizara imepanga kufanya matengenezo ya kilometa 38,384.90 za barabara kuu na barabara za mikoa pamoja na matengenezo ya madaraja 3,129”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Kuhusu vipaumbele vya Sekta ya Uchukuzi, Prof. Mbarawa ameeleza kuwa Serikali inakusudia kutekeleza miradi ya miundombinu ya reli ambapo ujenzi wa reli mpya ya SGR na ukarabati wa reli ya zamani ya MGR na TAZARA.
Waziri Mbarawa amesema katika kuimarisha bandari nchini Serikali imepanga kuboresha bandari zilizomo katika maziwa makuu ikiwemo bandari ya Bukoba, Kemondo bay, Mwanza South, Mwanza North, Kibirizi na Ujiji.
Serikali itaendelea na ununuzi wa mitambo ya kuongozea ndege na uendelezaji wa Chuo cha mafunzo ya usafiri wa anga ikiwa ni pamoja na mradi wa ununuzi wa rada mpya, na vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya hali ya hewa.
Kati ya zaidi ya shilingi Trilioni 3.5 zinazoombwa katika bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu takriban shilingi Trilioni 1.5 ni kwa ajili ya Sekta ya Ujenzi na shilingi Trilioni 2.086 kwa ajili ya Sekta ya Uchukuzi.