NI MGAO MKUBWA KISEKTA KUWAHI KULIPWA NCHINI
Na Mwandishi Wetu
Benki ya NMB imeweka rekodi mpya ya malipo ya gawio kwa wanahisa kwa mgao wa TZS 286 kwa kila hisa sawa na fidia jumla ya TZS bilioni 143.1 baada ya kupata ufanisi mkubwa wa mapato yanayotokana na riba mwaka jana.
Malipo hayo makubwa kitasnia yanatokana na wamiliki wa NMB ambayo ni moja ya benki tatu zinazoongoza kwa faida katika ukanda huu kuridhia na kuidhinisha kwa kauli moja bonasi hiyo Ijumaa iliyopita kwenye mkutano wao wa 23 wa kila mwaka uliofanyika kidijitali.
Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna, alisema mafanikio makubwa yaliyopatikana kiutendaji mwaka 2022 pia yameiheshimisha benki hiyo barani Afrika.
Kwa sasa taasisi hiyo kubwa kuliko zote za fedha nchini ni moja ya benki zinazoendeshwa kwa ufanisi mkubwa na kuongoza kwa mafanikio katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
NMB imepata umaarufu huo baada ya kufikia viwango vinavyostahili kwa kufanikiwa kuboresha uwiano wake wa Matumizi yasiyo ya Riba na Mapato Ghafi (CIR) hadi asilimia 42 kutoka kiwango cha asilimia 46 mwaka 2021.
Akiwatangaza kupitishwa kwa gawio hilo jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika mkutano mkuu huo, Bi Zaipuna aliwaambia waandishi wa habari kuwa mwaka 2022 ulikuwa wa mafanikio ambayo hawajawahi kuyapata ambapo gawio jumla lilikuwa ni ongezeko la asilimia 48 la mkupuo uliotangulia wa TZS bilioni 96.7.
Kwa kila hisa kupata nyongeza ya TZS 93 zaidi ya TZS 193 iliyolipwa mwaka jana (kwa ajili ya 2021), kiongozi huyo alisema hiyo ni hatua nyingine kubwa katika historia ya miaka 25 ya NMB ikiwa ni moja ya rekodi kadhaa za kiutendaji zilizowekwa mwaka jana.
“2022 ulikuwa mwaka wa kihistoria na mafanikio mengi kwa benki yetu. Tukiendelea kujiimarisha katika safari yetu tuliyoianza miaka 25 iliyopita, Benki ya NMB ilipata matokeo mazuri kuwahi kupatikana katika historia yake,” Bi Ruth alibainsiha.
Rekodi zilizowekwa ni pamoja na mapato jumla ya TZS trilioni 1.19 , faida ya TZS bilioni 429 baada ya kodi na thamani jumla ya mali zote iliyoongezeka na kuwa TZS trilioni 10.2.
Bi Zaipuna alibainisha kuwa mafanikio hayo makubwa ni matokeo ya utekelezaji mpango mkakati wao kwa nidhamu na kutimizwa kikamilifu kwa malengo yao ya kifedha na yasiyo ya kifedha
Aidha, alisema kuwa faida kubwa iliyopatikana ilitokana na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na riba kufuatia kuimarika kwa shughuli za ukopeshaji. Mchango wa mapato yasiyotokana na riba ulizidi kuiimarika kwa kuongezeka matumizi ya njia mbadala za kupata huduma hususani kidijitali.
Sababu nyingine alizotaja zilizochangia mafanikio na ufanisi huo ni umakini kwenye kuidhibiti mikopo chechefu na uangalifu mkubwa katika matumizi.
Wakati tengo la mikopo chechefu lilipungua wa asilimia 28 kutoka TZS bilioni 113 hadi TZS bilioni 81, gharama za uendeshaji ziliongezeka kidogo kwa asilimia tisa tu huku mapato yakikua kwa asilimia 21.
“Mapato yetu yatokanayo na riba hayakuongezeka kwa sababu ya kuongeza riba za mikopo bali kwa wingi wa shughuli za ukopeshaji. Nayo mapato yasiyotokana na riba yaliimarika kwa asilimia 31,” Bi Zaipuna alifafanua.
Kwa ujumla, NMB iliendeleza ukuaji thabiti wa mizania, kutokana na kuwa vizuri kimapato na kuimarika kimtaji. Ukopeshaji ulikua kwa asilimia 29 na kufikia TZS trilioni 6 ikilinganishwa na kiasi cha TZS trilioni 4.6 cha mwaka 2021.
Wingi wa amana nao ukaboreka zaidi kwa kuongezeka kwa asilimia 14 nakuwa TZS trilioni 7.6 kutoka TZS trilioni 6.6 za mwaka uliotangulia. Kutokana na kasi kubwa ya ukuaji wa mizania, jumla ya mali nayo haikuachwa nyuma ikakua kwa asilimia 18 kutoka TZS trilioni 8.7 na kuvuka kiasi cha TZS trilioni 10 kwa mara ya kwanza.
Ubora wa mali ulizingatiwa kwa karibu sana na kuzaa matunda. Hii ni baada ya hatari za hasara zinazotokana na wakopaji kushindwa kukamilisha marejesho kuendelea kupungua na kupelekea uwiano wa mikopo isiyolipika kufikia asilimia tatu kutoka asilimia 3.6.
“Matokeo chanya ya kiutendaji, sambamba na malipo ya gawio la TZS bilioni 143.1 yaliyoidhinishwa na wanahisa ni kielelezo cha mwelekeo pacha unaozingatia ukuaji wa muda mrefu na kupatikana kwa faida endelevu. NMB tunaendelea kuwa na mchango chanya kwa jamii kupitia uwekezaji wetu katika shughuli za kijamii na kiuchumi,” alisisitiza Bi Zaipuna.
“Kwa mwaka 2022, hatukupata tu matokeo mazuri ya kiutendaji na kuendelea kuandika histori ya kupata faida kubwa, bali pia tulilipa kodi stahiki serikalini na kuzidi kugusa maisha ya watu kwa kuwekeza katika shughuli za kijamii.” Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, Dkt Edwin Mhede, aliwaambia waandishi wa habari.
Kiasi jumla cha kodi zote ilizolipa NMB mwaka jana ni TZS bilioni 383 wakati bajeti ya TZS bilioni 6.2 yakuwajibika kwa jamii mwaka huu ni mara nne ya kiasi kilichotumika mwaka 2020.
Dk. Mhede alibainisha kwamba wanaamini kuwa mwaka huu wa fedha benki yao itaendeleza rekodi zake za ubora, ufanisi na mafanikio yaliyowapa tuzo zaidi ya 23 kwa mwaka 2022.
“Bodi ina matumaini makubwa na mustakabli wa maendeleo ya benki na imedhamiria kuhakikisha NMB inaendelea kuongoza na kuwa na mchango zaidi wa kijamii na kiuchumi,” alisisitiza.