NA ANDREW CHALE.
DAR ES SALAAM.
JUMUIYA ya Wazazi Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kipunguni imefanya tukio la kihistoria kwa kuzindua benki za mitaa (VICOBA) ilikufanya mambo makubwa kwa wananchi wake na kuepuka mikopo mingine iliyokuwa ikiwatesa ikiwemo mikopo ya ‘kausha damu’.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa VICOBA hivyo, Mgeni rasmi Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa, Sudi Kassim Sudi amepongeza Jumuiya hiyo huku akitaka jambo hilo liwe la kuigwa kwa WanaCCM wote nchini ilikusaidia juhudi za kuleta maendeleo kwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dkt.Samia Suluhu Hassan.
“Nimetembea nchi nzima ila jambo hili sijawahi sikia, zaidi nasikia mikopo mingine kausha damu na mengine, ila hii nimefurahishwa.
Hongereni sana Kipunguni tunataka watu wengine na jumuiya zingine zije kwenu kujifunza.” Amesema Sudi.
Aidha, amepongeza kwa namna ya Jumuiya hiyo kuweza kuanzisha kitu hicho na kuwa pamoja pasipo mafarakano ambapo amewashauri kuhakikisha wanafungua akaunti benki iliwaweze kupata kutanua mfuko wao.
“Niwapongeze tokea kuanza mpaka kufikia hatua hii bila kugombana.
Kinachotakiwa ni kuboresha mkafungue akaunti, akaunti hii itawasaidia, tunataka mwakani sio milioni 30 tena zaidi tusikie mna milioni 100…nyie mnatakiwa mtanue wigo kujiongeza kauli ya leo, “Mzigo ukue” ilikuwezesha hili jambo jema “bila mzigo maisha hakuna kitu, mzigo ndo Habari ya mjini, nawashukuru na kuwasifu sana, sisi tutawashauri wenzetu ngazi ya wilaya, mkoa na taifa kuja hapa kujifunza.” Amesema Sudi.
Aidha, Jumuiya hiyo mbali ya kufungua VICOBA, pia wamezindua mradi wa kuimarisha na kuboresha mawasiliano kwa kuwauzia wanachama wao simu za mkononi kwa mkopo nafuu ilikurahisha mawasiliano ambapo mgeni rasmi aliahidi kuwapa sapoti ya kuchangia mtaji bidhaa za simu.
“Naomba nitawasaidia upande wa simu nitaona namna ya kusaidia kupata bei ya chini ili mueze kununua kwa kiasi hicho hicho cha chini.
Mie ni mdau upande huu, nitawasaidia kupata simu za chini ili kila mtu anunue, mkiwa tayari mtaniletea bajeti yenu kuona nachangiaje” amesema Sudi.
Amesema kwa hatua hiyo imewapa somo na anahakika jambo hilo linaenda kuwa kubwa: “Tunataka kufanya jambo kubwa mpaka Rais wetu Mhe Samia Suluhu Hassan aje hapa aone panajambo, tunataka muendelee na umoja huu.
“Sisi tunapenda kuona Jumuiya yetu ya wazazi inachangamka Jumuiya yetu ya Dar es Salaam kwa sasa imechangamka,
Inafanya vizuri kwa kila idara, hivi ndivyo tunavyotaka Jumuiya ziwe.” Amesema Sudi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Peter Mkufya akitoa taarifa ya VICOBA Kipunguni amesema walianzisha wazo hilo kuwakwamua wanchama na mikopo mingine ikiwemo ya “Kausha damu” ndani ya Kata yenye Mitaa 6 ya Mtaa wa Matawi, Machimbo, Wazalendo, Kipunguni B, na Mtaa wa Kitinye ambapo kila mtaa wakahamasisha na kuunda benki hizo za mtaa (VICOBA) kwa kuanza kiwango kidogo na sasa wameweza kufikisha zaidi ya Milioni 30.
Mbali ya kuzindua VICOBA kipunguni, huduma ya mawasiliano, pia wamezindua rasmi kitabu cha JITAMBUE ambacho kitasaidia kumsaidia mtoto ikiwemo kujifunza katika hatua mbalimbali pamoja na kupambana na unyanyasaji.
“Kitabu hichi cha Jitambue ni kwa vijana, watoto na Wanafunzi ambapo tunataka kuwafikia wengi zaidi kwa kushirikiana na wabia ndani ya Kata na nje, ikiwemo Jumuiya za UVCCM, UWT, pamoja na asasi zisizo za Kiserikali.
Kitabu kina mbinu 48 za kupinga ukatili, Mbinu za kitaaluma ikiwemo kushinda mitihani ya shule, Vyuoni na maishani.
Aidha, katika uzinduzi huo, waliweza kufanya Harambee ya kawaida na kufanikiwa kukusanya kiasi cha Fedha zaidi ya Milioni tatu, kutoka kwa viongozi mbalimbali ikiwemo viongozi waalikwa na wa matawi ndani ya chama hicho.