Home KITAIFA Serikali ya Z’bar yapongeza Miaka 25 ya Mafanikio NMB

Serikali ya Z’bar yapongeza Miaka 25 ya Mafanikio NMB

Google search engine
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa tatu kushoto) akimkabidhi jezi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah (wa tatu kulia) zilizotolewa na Benki ya NMB kwa ajili ya vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye hafla ya chakula cha jioni na wajumbe wa baraza la wawakilishi lenye lengo la kusherekea miaka 25 ya Benki ya NMB na kudumisha ushirikiano baina ya NMB na Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar (BLW), iliyofanyika Jijini Zanzibar. Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dk. Edwin Mhede (wa pili kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa (wa pili kulia), Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Zubeir Ali Maulid (kulia) wakishuhudia na kushoto ni Meneja wa Biashara NMB Zanzibar, Naima Said Shaame
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa tatu kushoto) akimkabidhi mfano wa madawati 407 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah (wa tatu kulia) zilizotolewa na Benki ya NMB kwa ajili ya shule mbalimbali visiwani Zanzibar kwenye hafla ya chakula cha jioni na wajumbe wa baraza la wawakilishi lenye lengo la kusherekea miaka 25 ya Benki ya NMB na kudumisha ushirikiano baina ya NMB na Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar (BLW), iliyofanyika Jijini Zanzibar. Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dk. Edwin Mhede (wa pili kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa (wa pili kulia), Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Zubeir Ali Maulid (kulia) wakishuhudia na kushoto ni Meneja wa Biashara NMB Zanzibar, Naima Said Shaame

NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imeipongeza Benki ya NMB kwa mafanikio yaliyotukuka katika kipindi cha miaka 25 ya kuhudumia Watanzania, na kuwa haishangazwi na rekodi za kihistoria za mapato na faida zinazowekwa na benki hiyo, kwani inatambua fika kuwa siri ya mafanikio hayo ni mvuto wake kwa jamii unaotokana na kuwathamini Watanzania.

SMZ, imebainisha kuwa inaheshimu, kujali na kuthamini mchango endelevu wa taasisi hiyo katika kustawisha Sekta za Kimkakati visiwani humo, hasa za elimu, afya, utalii na uvuvi, huku ikizitaka taasisi za fedha nchini sio tu kuiiga NMB, bali kujifunza kutoka kwa vinara hao waliopitia hatua mbalimbali hadi kufikia walipo.

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, wakati wa hafla ya chakula cha jioni pamoja na Baraza la Wawakilishi lililoambatana na zoezi la lenye nia ya kusherekea miaka 25 ya utoaji huduma ya Benki ya NMB na kudumisha ushirikiano baina ya NMB na Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar (BLW) ambapo awali ilitanguliwa na Bonanza la michezo, iliyofanyika Jumamosi usiku hapa Zanzibar.

Bonanza hilo lililotambulika kama NMB Baraza Sports Bonanza, limetumiwa na benki hiyo kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 ya huduma za fedha Tanzania, sambamba na kulitumia kutoa msaada wa madawati 407 yenye thamani ya Sh. Mil. 43 kwa ajili ya shule nne za Zanzibar na viti 100 na meza 100 za Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Hayati Karume (KIST).

Akizungumza katika hafla hiyo, Abdullah alisema SMZ na BLW wanajivunia sana ushiriki na mchango wa NMB katika maendeleo ya Zanzibar, huku akifafanua kuwa benki hiyo imeweka msukumo mkubwa katika kuchagiza ustawi wa maendeleo ya Wazanzibar, huku akiitabiria mafanikio makubwa zaidi kitaifa na kimataifa.

“Niwahakikishie tu kwamba NMB mtapata mafanikio makubwa mno, kwani mmekuwa vinara wa kusaidia utatuzi wa changamoto mbalimbali za kijamii, mchango wenu kwa jamii ya watu wa chini kabisa ni mkubwa na sishangai wala kujiuliza ukubwa wa mapato na faida yenu unatokana na nini, siri ya mafanikio yenu ni kujali jamii inayowazunguka.

“Taasisi zingine za fedha zina mambo mengi ya kuiga kutoka NMB, zaidi zinapaswa kujifunza namna sahihi ya kujikubalisha kwa Watanzania,” alisema Abdullah, huku akiwataka Wazanzibar kutumia fursa za kiuchumi ilizonazo benki hiyo, ikiwamo kukopa kwa malengo na kurejesha kwa wakati bila kushikizwa ili kutanua faida, hivyo kukuza fungu la Programu ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI).

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa NMB, Ruth Zaipuna, alikiri kufurahishwa na ushirikiano mkubwa inaopata benki yake kutoka SMZ na BLW, huku akiweka ahadi ya kudumisha mashirikiano hayo, ili kuharakisha ukuaji uchumi wa Zanzibar.

Aliieleza kuwa wanajisikia fahari kwa aina ya mafanikio waliyopata katika kipindi cha miaka 25, huku akikiri kwamba haikuwa kazi rahisi kuyafikia tangu 1997 walipokuwa wakitambulika kama Benki ya Makabwela na kwamba ilikuwa ni safari ndefu na ngumu.

“Ilikuwa ni safari ngumu, tuliyoianza na matawi 97 tu huku huduma karibu zote zikipatikana matawini, lakini sasa tuna matawi 229, ATM na mawakala Zaidi ya 20,000, pamoja na mifumo ya kidijitali inayowezesha kupata kila huduma nje ya matawi, ikiwamo kufungua akaunti na kukopa ‘Mshiko Fasta’ bila dhamana yoyote.

“Tukaona tuje kusherehekes miaka yetu 25 ya mafanikio pamoja nanyi ambao mmetoa mchango mkubwa kutufikisha hapa. Tuna matawi matatu hapa Zanzaibar na mwaka huu kabla haujaisha tutafungua mengine matatu huko Nungwi, Paje na kwingineko,” alisema huku akijivunia mikataba na makubaliano mbalimbali na taasisi na mamlaka za SMZ.

“Tuna ushirikiano na Mamlaka yay a Serikali Mtandao (E GAZ) ya kutoa suluhishi za malipo na makusanyo kwa taasisi za SMZ, tunashirikiana pia na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), kutengeneza mifumo ya kufuatilia taarifa na kuhudumia wawekezaji, pamoja makubaliano na Mamlaka ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe katika kuhifadhi Bustani ya Forodhani ambayo ni moja ya vivutio vya kitalii,” alifafanua.

Zaipuna aliiahidi Serikali ya Zanzibar ushirikiano endelevu katika kuharakisha ukuaji Uchumi wa Buluu, huku akifichua kuwa mwaka huu NMB imetenga Sh. Bilioni 6.2 kurejesha kwa jamii, zikiwamo Sh. Bilioni 2 za Kampeni ya Kitaifa ya Upandaji miti, sanjari na elimu ya mazingira kwa wanafunzi wa Shule za Msingi 189 zinazoshiriki Shindano la ‘Kuza Mti Tukutuze’

Akaongeza kuwa, kiasi hicho cha Sh. Bilioni 6.2 ni Zaidi ya mara tatu ya ilichotumia mwaka 2021 cha Sh. Bilioni 2 za Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), sasa CSI, huku mwaka 2022 ikitumia kiasi cha Sh. Bilioni 2.9, lakini mafanikio ya faida baada ya kodi ya Sh. Bilioni 429, yakawezesha kuongeza kwa fungu la kurejesha kwa jamii.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Dk. Edwin Mhede, miongoni mwa siri zilizowawezesha kupata mafanikio hayo ya kupigiwa mfano katika Sekta ya Fedha Tanzania ni pamoja kuiishi falsafa ya kutoa suluhishi za kifedha kwa jamii na kwamba faida kubwa iliyopata mwaka jana ni uthibitisho wa huduma bora na rafiki walizonazo.

“NMB tutaendelea kugusa maisha ya watu wa kada zote, kwani tunaamini tuna fursa za kutosha kuchagiza ustawi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Mafanikio yetu pia yametokana na uwepo wa mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali ambayo inamiliki hisa asilimia 31.8, lakini pia watumishi wenye weredi, waadilifu na makini wanaoifanya NMB kuwa Benki Salama Zaidi ya kutunza fedha,” alisema. 

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here