Home KITAIFA TFS YAENDELEA KUJIZATITI KUKABILIANA NA MAJANGA YA MOTO MISITUNI

TFS YAENDELEA KUJIZATITI KUKABILIANA NA MAJANGA YA MOTO MISITUNI

Google search engine

NA MWANDISHI WETU

Wakala  wa huduma  za misitu Tanzania (TFS) kupitia Shamba la  Miti la Serikali Sao Hill lililopo Wilayani ,Mufindi Mkoani Iringa, wamefanya usaili wa ajira kwa vikosi vya kupambana na kuzuia Matukio  ya moto ambapo jumla ya  Vijana 192 watanufaika  na ajira hizo.

Akizungumza wakati wa usaili wa vikosi vya kupambana na kuzuia matukio ya moto , Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Saohill PCO. Tebby Yoramu amesema katika idadi hiyo jumla ya vijana 180 watakuwa katika vituo vya kazi (Standby Crew) katika vituo vyote vya Tarafa nne za Shamba na vijana 12 watakuwa katika mitambo maalumu inayotumika katika kuzima moto.

“Imetulazimu kufanya zoezi hilo la usaili ili tuone namna nzuri tutakavyowapata wale vijana wataofanya kazi kulingana na vigezo tulivyotoa na pia tunahitaji vijana ambao wapo timamu,wenye afya njema, ujuzi na wenye uwezo wa kufuata maelekezo, kuchambua na kutekeleza maelekezo hayo kulingana na vile inayotakiwa.” Amesema Kaimu Mhifadhi Mkuu

Aidha Kaimu Mhifadhi Mkuu ameongeza kuwa matukio ya moto yamekuwa yakipungua kutoka mwaka mmoja na mwingine hivyo TFS kupitia Shamba la Miti SaoHill wana matarajio makubwa kwamba kwa mwaka huu pia matukio ya moto yatapungua kulinganisha na mwaka wa nyuma na kuendelea kutoa wito kwa wananchi kuwa na ushirikiano mkubwa katika kudhibiti matukio ya moto unaoathiri misitu.

Kwa upande wake Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba upande wa Uendelezaji Msitu , SCO. Said Singano amesema kuwa TFS kupitia Shamba limekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya moto usiokuwa na madhara na pia kama shamba limekuwa likitoa miche kwa wananchi wanaolizunguka kwa ajili ya kupanda kwenye maeneo yao, hivyo ni wakati sasa kwa wananchi kushirikiana kwa pamoja katika kuitunza miti hiyo iliyopandwa.

Aidha amewataka wananchi kuhakikisha wanafuata taratibu zote za matumizi ya moto katika shughuli zao mbalimbali ikiwemo shughuli za maandalizi ya mashamba, urinaji wa asali na shughuli nyingine zinazorumika moto ili kuondoa matukio ya moto msituni yanayoleta hasara katika uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo Mkuu wa kitengo cha Ulinzi wa misitu dhidi ya majanga mbalimbali ikiwemo ya moto , CO I . Murya Sawa amesema kuwa kitengo cha Ulinzi wa Msitu wamejipanga vyema kuhakikisha matukio ya moto katika misitu yanapungua kwani wamejiandaa vyema na wamefanya maboresho ikiwemo maandalizi ya vifaa vinavyotumika ikiwemo majembe, mipira ya kuzimia moto sambamba na kuongeza na kuboresha minara ya kuangalia viashiria vya moto katika maeneo yanayolizunguka shamba.

Usahili huu unatarajiwa kuendelea katika tarafa nyingine za shamba ili kuhakikisha wanafikia idadi ya iliyopangwa.

Shamba la Miti SaoHill ni miongoni mwa mashamba 24 ya miti ya kupandwa yanayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii lenye ukubwa wa hekta 135,903

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here