NA ARODIA PETER
-DAR ES SALAAM
Wazazi nchini wameaswa kuwa makini na matumizi ya teknolojia bila kuathiri usalama na makuzi ya watoto kwa kutumia Tehama.
Wito huo umetolewa leo na baadhi ya watoto katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto Afrika yaliyofanyika leo Juni 16,2023 katika Shule ya Sekondari Nguvu mpya Chanika Ilala mkoani Dar es Salaam.
Wakisoma risala kwa niaba ya wenzao kwenye maadhimisho hayo, Bestina Bosco na Suleimani Juma kutoka Shule ya Msingi Mzambarauni walitoa angalizo kwa wazazi kuwa karibu na watoto kwa kufuatilia nyendo zao wanapowaruhusu watoto ambao kisheria hawaruhusiwi kumiliki wala kutumia simu au vifaa vya kidigitali.
Walivitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja kompyuta, vishikwambi, intaneti kuwa visiruhusiwe bila ridhaa ya wazazi.
“Pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kutunga sera, sheria na miongozo mbalimbali ya ulinzi, malezi na makuzi ya mtoto, bado mtoto amekuwa mhanga wa ukatili, udhalilishwaji na unyanyaswaji mitandaoni.
“Aidha wazazi kwa kujua au kutokujua wamekuwa wakituma picha za watoto wao kwa malengo ya kupata maoni au kupendwa.” Ilisema sehemu ya risala hiyo.
Kwa upande wake, Mratibu wa kuunganisha familia wa SOS Village Dar es Salaam, Kennedy Mashema amesema maadhimisho hayo yamefanywa na mashirika zaidi ya 10 yanayotetea haki za watoto kwa usimamizi wa shirika hilo.
Amesema kwa sasa SOS Village wanaandaa program mbalimbali kuhusu sekta ya tehama inavyoweza kuchochea maendeleo bila kusababisha ukatili kwa watoto.
Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Ilala ambaye aliwakilishwa na Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Chalangwa Selemani aliwaasa wazazi kuacha kutuma picha za watoto wao mitandaoni wakidhani ni kuwapenda.
Alisema hatua hiyo ni sawa na ukatili na haikubaliki kwani ni kinyume cha sheria zinazolinda watoto.
Chalangwa pia aligusia vitendo vya ukatili vinavyoendelea katika jamii na hata shuleni na kuathiri zaidi watoto kwa kiwango kikubwa.
Ili kukabiliana na ukatili wa aina mbalimbali kwenye jamii Chalangwa ameshauri kuwepo kwa masanduku ya maoni shuleni ambapo watoto wataruhusiwa kila mmoja kwa wakati wake kuandika vitendo vya ukatili anavyokumbana navyo katika mazingira ya shuleni na nyumbani.
Maadhimisho ya Siku ya mtoto Afika mwaka huu 2023 imebaba kauli mbiu inayosema “Zingatia usalama wa mtoto katika Ulimwengu wa kidigitali.
Katika maadhimisho hayo mashirika zaidi ya 10 yanayofanyakazi na Taasisi ya SOS Village yaliandaa tamashasha hilo kwa kushirikisha watoto wanaosoma katika baadhi ya shule mbalimbali wilayani humo.
Siku ya mtoto Afrika huadhimishwa tarehe 16 Juni kila mwaka kuwakumbuka watoto waliouawa huko Soweto Afrika Kusini kwa ubaguzi wa rangi wakati wa utawala wa makabulu.