Na Mwandishi Wetu
-Zanzibar
Benki ya NMB imetangaza kuendeleza dhamira yake ya kusaidia ukuaji wa sekta ya utalii pamoja na Ajenda ya Uchumi wa Bluu ikiwa ni utelelezaji wa mkakati wake wa muda mrefu unaolenga kuunga mkono jitihada za kunaongeza mchango wa sekta hizo katika maendeleo ya kiuchumi visiwani Zanzibar kwa ujumla.
Akizungumza na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan wakati wa maonesho ya pili ya Chakula cha Baharini visiwani Zanzibar yaani ‘Zanzibar Sea Food Exhibition 2023’ yaliyofanyika mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Idara ya Biashara za Serikali Vicky Bishubo alisema kwa miaka mingi sasa, benki hiyo imekuwa ikishirikiana kwa ukaribu na Serikali ya Zanzibar katika kuimarisha ukuaji sekta ya utalii na ajenda ya Uchumi wa Bluu ilikuchangia ukuaji wa Pato la Taifa la Zanzibar (GDP).
“Sisi kama benki ya NMB, tumeanzisha masuluhisho mbalimbali za kibenki ili kuchangia juhudi za Serikali katika kuinua mchango ya sekta za utalii na Ajenda ya Uchumi wa Bluu ikiwa ni utekelezaji wa azma yetu ya kuhakikisha kuwa sekta hizo zinachangia zaidi katika uchumi wa Zanzibar kwa ujumla,” alisema.
Bishubo alibainisha kuwa benki hiyo tayari imesaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Shirika la bandari Zanzibar (ZPC) ili kuanzisha mfumo jumuishi yaani ‘one-stop centre’ ambao pamoja na mambo mengine utawawezesha wafanyabiashara kulipa kodi kwa kutumia mfumo wa udhibiti namba yaani ‘control number’.
“Mfumo huu pamoja mambo mengine unalenga kurahisisha mchakato wa malipo na kwa kiasi kikubwa utaokoa muda kwa wafanyabiashara na kuhakikisha uwazi kwa serikali katika suala zima la ukusanyaji wa mapato,” alisema.
Aliongeza kuwa benki hiyo pia imeshirikiana na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kuunda mfumo wa pamoja ambao unalenga kurahisisha mchakato wa uwekezaji visiwani Zanzibar.
“Mfumo huu unatoa fursa kwa wawekezaji watarajiwa kuomba huduma kutoka kwa taasisi zote zinazoshiriki katika uwezeshaji wa uwekezaji hivyo sio tu kurahisisha mchakato mzima wa uwekezaji bali pia kuboresha ufanisi wa uendeshaji,” Bishubo alisema.
Bishubo alisema katika juhudi za benki hiyo kukuza ujuzi wa masuala ya fedha visiwani Zanzibar, tayari yake imetoa mafunzo ya kifedha kwa zaidi ya watu 10,000 wakiwemo wafanyabiashara wadogo na za Kati (SMEs) katika sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo, uvuvi na nyinginezo visiwani Zanzibar.
Alibainisha kuwa benki hiyo kwa sasa ina mtandao wa matawi matatu Unguja, Zanzibar na mawakala zaidi ya 200 pamoja na zaidi ya mashine 20 za Kutoa Pesa (ATM).
“Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma na bidhaa zetu, tulipokea maombi mengi ya kufungua tawi jingine Unguja Kusini na kama sehemu ya utekelezaji wa falsafa yetu ya ‘karibu yako’, maandalizi ya kukamilisha tawi hilo yapo katika hatua za mwisho na tawi hilo jipya litazinuliwa na kuanza kufanya kazi hivi karibuni,” Bishubo aliongeza.
Naye Mkuu wa Mtandao wa Matawi ya Benki ya NMB, Donatus Richard wakati wa hafla hiyo alibainisha kuwa benki hiyo ina suluhu mbalimbali kwaajili ya kuwezesha watalii mbalimbali wanaotembelea visiwa vya Zanzibar hasa wale wanaotoka Mashariki ya Mbali.
“Tunayo masuluhisho na bidha mbalimbali ambazo tumeanzisha kwa makusudi kuwa ajili ya ya watalii’ ikiwa ni pamoja na kuanzisha mashine mbalimbali za ‘Point of Sales’ (POS) katika vivutio vyote vikubwa vya watalii visiwani Zanzibar ilikuwawezeza watalii kupata huduma za kibenki bila vikwazo. Kupitia juhudi zetu, watalii hasa kutoka Mashariki ya Mbali sasa wanaweza kupata huduma za kwa kutumia kadi za Union Pay,” alisema Richard.
Rais wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan wakati wa hafla hiyo aliipongeza benki hiyo kwa jitihada zake za kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali za kuongeza ushirikishwaji wa kifedha nchini kote.
“Nachukua fursa hii kuipongeza benki ya NMB kwa jitihada zake za kuendela kuunga mkono juhudi mbalimbali za ujumuishaji wa kifedha. NMB oyee,” alisema Dk. Samia.