Na Mwandishi Wetu
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema haijazuia biashara ya mazao ya Misitu huku ikiwataka wafanyabiashara wa mazao ya misitu kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha kuna kuwa na usawa katika biashara hiyo pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali hiyo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kibaha Vijijini, Michael Costantino Mwakamo, aliyetaka kujua kauli ya Serikali juu ya Wafanyabiashara wa mazao ya misitu wanaozuiwa kufanya biashara na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
”Natoa rai kwa wafanyabiashara wote wenye nia njema ya kuvuna au kufanya biashara ya mazao ya Misitu wafuate Sheria, Kanuni na taratibu zilizowekwa” amesisitiza Masanja .