Na Andrew Chale, Zanzibar.
FILAMU ya ‘Nakupenda’ inatarajiwa kuoneshwa jioni ya leo Juni 27, katika tamasha la Kimataifa la Filamu za Nchi za Jahazi [ZIFF], ndani ya Ngome Kongwe, Unguja, Zanzibar.
Filamu hiyo ya Nakupenda iliotayarishwa na kuongozwa na Juma Saada, inaelezea Hadithi ya mapenzi ya Bibi na Babu waliopendana toka utotoni na kushindwa kuambiana na baadae kuja kukutana uzeeni na kila mmoja kuamsha hisia zake kwa mwenzie.
Juma Saada amesema kuwa, ametoa wito kwa wadau kujitokeza kuishuhudia filamu hiyo kwani ina mambo mengi ikiwemo kuelimisha na kuburudisha pia.
‘’Leo ni siku maalumu mapenzi kuyaenzi kwa hadithi nzuri iitwayo ‘Nakupenda’ itakayosimuliwa Ngome kongwe hapa Zanzibar katika jukwaa la ZIFF.
Hadithi inavutia, inatuvuta, njoo tusimuliwe pamoja mapenzi’’ amesema Juma Saada.
Aidha, amewataja wahusika wakuu kuwa ni pamoja na Isaya Ryoba aliyetumia jina la Mzee Sakilu pamoja na Tekla Mjata ametumia jina la Bi.Nafu ambao ni miongoni mwa waigizaji filamu wakongwe na mvuto katika uigizaji wa hutu uzima.
Juma Saada amesema kuwa, filamu hiyo imehusisha timu kubwa na kila mmoja ameweza kucheza nafasi yake ambapo anaamini watu watakapoiona wataifurahia kwani imefanyiwa katika mazingira tofauti ya kupendeza ndani ya Tanzania ikiwemo Morogoro katika miji ya Kiloka na Kiziwa, na Tanga katika maeneo ya Lushoto-Amani na Tanga mjini.
Filamu ambayo inaelimisha, burudisha, sisismua ambayo kila mmoja ataifurahia, sio hadithi ya mapenzi, ni hadithi inayoyahusu mapenzi’’ Amemalizia muongozaji wa filamu hiyo, Juma Saada