NA MWANDISHI WETU
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeanza kufanyia maboresho Kanuni na Mwongozo wa Biashara ya Kaboni za mwaka 2022 ili ziweze kuwatambua na kuwanufaisha wakulima na wafugaji nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis wakati akijibu maswali ya Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Jacqueline Ngonyani Msongozi bungeni jijini Dodoma leo Juni 28, 2023, amesema kanuni hizo zinalenga kuhakikisha kuwa jamii, wadau mbalimbali wanaohusika na biashara hiyo ikiwa pamoja na Serikali kunufaika kikamilifu kutokana na faida zake.
Aidha, Khamis ameeleza kuwa Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kutoa elimu ya mazingira kwa umma ikiwemo ya Biashara ya Kaboni.
Amesema ni matumaini ya Serikali kwamba, kupitia jitihada hizo wananchi wataweza kupata uelewa na kunufaika na biashara hiyo wakiwemo wakulima na wafugaji.
Naibu waziri amefafanua kuwa Biashara ya Kaboni ni moja ya mbinu za kupunguza uzalishaji wa Gesijoto (Mitigation) ambayo iliridhiwa katika itifaki ya Kyoto ikizitaka nchi wanachama kupunguza uzalishaji wa gesijoto iliyorundikana angani.
Hali kadhalika amesema kuwa biashara hii ipo katika masoko ya aina mbili ambayo ni Soko la hiari/huria (Voluntary Carbon Market) na Soko la Umoja wa Mataifa (Official Carbon Market).
Pamoja na Mwongozo huo, tayari Ofisi ya Makamu wa Rais imetoa elimu kwa makundi mbalimbali wakiwemo, Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Wizara zote za kisekta pamoja na taasisi zake, wakuu wa wilaya wote, wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mkoa na kwa wadau mbalimbali.
Itakumbukwa Juni 19, 2023 Ofisi ilitoa semina kwa akifunga warsha wahariri wa vyombo vya habari iliyolenga kujenga uelewa kuhusu Kanuni na Mwongozo wa Biashara ya Kaboni.