NA MWANDISHI WETU
Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia,Felix Wandwe amewapongeza watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na taasisi zake za CFR, AICC na APRM-TANZANIA kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuelimisha umma katika Maeonesha ya Kimataifa ya Biashara ya Dar Es Salaam, maarufu sabasaba yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar Es Salaam.
Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 10 Julai 2023 alipotembelea Banda la Wizara hiyo lililopo kwenye Jengo la Karume.
“Nimeona kupitia vyombo vya habari na mitandao ya Jamii namna mlivyokuwa mkiwahudumia wananchi kwa weledi wa hali ya juu, hongereni sana,” Wandwe alipongeza.
Aliongeza kuwa anapongeza uongozi wa Wizara kwa uamuzi wake wa kukaa Banda moja na taasisi zake, jambo ambalo limeongeza ufanisi katika kuhudumia na kutoa fursa kwa watumishi kujifunza na kubadilishana uzoefu.
Amesema uamuzi huu uendelee katika Maonesho yajayo na anaamini utaleta tija kubwa, kwa sababu dalili zimeonekana kwenye Maonesho haya.