NA MWANDISHI WETU
-ZANZIBAR
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amewahakikishia Wabunge wa Zanzibar kuwa Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMTZ) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zitaendelea kuweka mifumo wezeshi ya upatikanaji wa fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo ili kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inatekelezwa na kukamilika kwa wakati.
Waziri Jafo ameyasema hayo leo Julai 11, 2023 Mjini Zanzibar wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku moja kwa Wabunge na Watendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhusu usimamizi wa fedha za mfuko wa Jimboyaliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi Ndogo za Bunge Tunguu, Mjini Zanzibar.
Amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka miwili wa Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan na ile ya Awamu ya Nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, Zanzibar inaendelea kupokea kiasi kikubwa cha fedha za utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayolenga kuleta matokeo channya kwa wananchi
Waziri Jafo amesema ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inaleta matokeo yaliyokusudiwa, Serikali zote mbili zitaendelea kuweka mkazo katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha za miradi kwa kuwa ndio kipaumbelecha viongozi katika kuwaletea maendeleo wananchi wa pande zote za Muungano.
“Jambo la matumizi ya mifumo ni suala la kidunia, kwa mfano kwa sasa kuna mfumo wa TANEPS katikamanunuzi, mfumo huu hatuwezi kuepukana nao, suala la msingi na muhimu ni kuhakikisha kuwa vipaumbele vya miradi tuliyoipanga kuitekeleza katika majimbo yetu inazingatia kanuni taratibu zilizopo” amesema Dk. Jafo.
Aidha Dk. Jafo amewataka Wabunge kuwa wabunifu katika kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo inayoelekezwa katika majimbo yao kupitia fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo na kuongeza kuwa Serikali zote mbili zitahakikisha kuwa fedha zote za miradi ya maendeleo zinafika kwa wakati na kutekeleza miradi yote iliyokusudiwa kuwanufaisha wananchi.
Waziri Jafo amesema wapo baadhi ya wabunge walioomba kubadilishwa kwa sharia ya mfumo wa jimbo ikiwemo kutoa mamlaka kwa Wabunge kuwa maafisa masuhuli wa fedha za mfuko ambapo amesema jambo ambalo ni gumu kutekelezeka kwa mujibu wa taratibu za sheria zinazosimamia mfuko huo.
Akifafanua zaidi, Waziri Jafo amesema ni ukweli ulio wazi kuwa fedha za mfuko wa jimbo zimekuwa na mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya majimbo na hivyo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zitaendelea kuratibu ushauri wa kitalaamu wa namna ya kuhakikisha fedha za mfuko zinawafikia walengwa.
Waziri Jafo amewataka Watendaji na wabunge kuimarisha mahusiano na ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao na kutokuwa kikwazo katika ufanisi wa utekelezaji wa maendeleo inayosimamiwa na fedha za mfuko wa jimbo katika maeneo yao ya kazi kwani dhamira ya Serikali ni kuwaletea maendeleo wananchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis amesema Serikali itahakikisha inafanyia kazi hoja na maoni yote ya Kamati za Mfuko wa Jimbo kwa kusimamia kikamilifu utoaji wa fedha kwa kuwa manufaa ya miradi hiyo tayari yameonekana kwa kuleta matokeo jamii katika jamii mbalimbali.
“Tunatambua kuwa zipo baadhi ya changamoto kadhaa za fedha za mfuko wa jimbo ikiwemo makato ya kodi, Serikali itahakikisha kuwa suala hilo linashughulikiwa ili ifike wakati kwa fedha za mfuko wa jimbo zinaondolewa kodi na kumaliza kilio hiki cha muda mrefu cha Wabunge,” amesema Khamis
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Zanzibar, Haji Amour Haji aliishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo ni mwanzo wa hatua muhimu za Serikali zote mbili inalenga kushughulikia changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika usimamizi wa fedha za mfuko wa jimbo.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Dk. Islam Seif Salum amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) kwa pamoja zimeendelea kushughulikia changamoto mbalimbali za mfuko wa maendeleo ya jimbo ikiwemo suala la upatikanaji wa fedha kwa wakati.
Aidha Dk. Salum amesema matumizi ya mifumo ya kamwe hayawezi kuepukika usimamizi wa fedha za utekelezaji wa miradi ya fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo kwani dunia ipo katika hatua kubwa za mabadiliko ya sayansi na teknolojia na kuongeza kuwa ni wajibu na Wabunge na watendaji kuendelea kuzingatia uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kupitia fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo.
Mafunzo hayo ya siku moja yalihudhuliwa na wabunge wa majimbo 50 ya uchaguzi ya Zanzibar yakiwemo majimbo 32 ya upande wa Unguja na majimbo 18 ya upande wa Pemba. mafunzo hayo yanatarajia kufanyika pia katika majimbo ya Pemba kuanzia tarehe 12 Julai, mwaka huu.