*YAKOPESHA SHILINGI BILIONI 317 KWA WAKULIMA, UKWASI WAPAA
NA MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege, amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa benki hiyo mwaka 2015 uwezo wa benki hiyo umekuwa ukikuwa na kufikia kupokea Shilingi bilioni 317 kutoka kwa serikali kwa ajili ya kuwezesha wakulima na wafugaji nchini.
Hayo ameyasema leo Alhamis Julai 13, 2023 wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari ikiwa ni utaratibu mpya uliowekwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina katika kueleza mafanikio na changamoto za mashika ambayo yapo chini yake.
Nyabundege amesema lengo la kuanzishwa kwa Benki ya TADB ni pamoja na kuchangia utoshelevu na usalama wa chakula nchini pamoja na kuchagiza mageuzi ya kilimo kutoka kwenye kilimo cha kujikimu na kwenda kwenye kilimo cha biashara kitakachochangia kupunguza umaskini na kukuza uchumi wa nchi.
Amesema tangu kwa benki hiyo mwaka 2015 ilianza na mtaji wa Shilingi bilioni 60 uliotolewa na serikali ya awamu ya tano na tangu alipoingia madarakani Rais wa Awamu ya Sita, Dk. Samia Suluhu Hassan aliiongezea mtaji wa mkupuoa Mwaka 2021 na kuipa benki hiyo Shilingi Bilioni 208 kwa kubadilisha fedha hizo kama mkopo kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na kuwa mtaji.
“Kufuatia kupatikana kwa mtaji huo, TADB imefanikiwa kujiendesha kiufanisi, kutengeneza faida na kukuza mtaji hadi kufikia Shilingi Bilioni 302.5 ambazo zimerekodia hadi kufikia Desemba 31, 2022 sawa na ongezeko la asimilia 404.17 ikilinganishwa na mtaji uliowekwa wakati benki inaanzishwa.
“TADB inatoa mikopo ya muda mfupi chini ya miaka miwili, muda wa kati miaka miwili hadi mitano na muda mrefu wa miaka mitano hadi 15 kwa njia ya moja kwa moja. aidha TADB inachagiza utoaji wa mikopo kupitia benki washirika kwa kutoa dhamana kupitia mfumo wa dhamana kwa wakulima wadogo,” amesema Nyabundege.
Akizungumzia mtandao wa benki hiyo, amesema kuwa wamefanikiwa kufungua ofisi Kanda ya Ziwa katika mkoa wa Mwanza ambayo inahudumia mikoa Mwanza, Kagera, Shinyanga, Simiyu, Mara na Geita huku Kanda ya Kati ikihudumia mikoa ya Dodoma na Singida.
Pia benki hiyo imefungua ofisi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Mashariki na Kanda ya Kusini ambayo imefunguliwa hivi karibuni.
Nyabundege, akizungumza thamani ya kitabu cha benki thamani ya kitabu hicho kuwa imeendelea kukua, kutoka Shilingi bilioni 61.6 mwaka 2015 hadi Shilingi bilioni 447.9 katika mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 627.1.
Mkurugenzi huyo akizungumzia kuanzishwa kwa Dawati Maalum la Mikopo ya Wavuvi, amesema benki hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatekeleza mradi wa Blue Economy for Growth ambao lengo lake ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya mwani na uvuvi wa samaki kwa kutoa mikopo ya gharama nafuu.
“Mikopo hiyo inatumiwa kwa ajili ya ununuzi wa boti za kisasa, ujenzi wa vizimba vya kufugia samaki, kuendeleza kilimo cha zao la mwani na kutoaji ushauri wa kitaalamu. Mradi huu unatekelezwa katika mikoa inayozungukwa na maziwa makuu kwa maana Ziwa Victoria na Tanganyika, Rukwa na Nyasa pamoja na mikoa inayopakana na Bahari ya Hindi.
“Benki imeweka dawati maalumu la mikopo yenye riba ya asilimia sifuri kwa ajili ya mradi huo na jumla ya Shilingi bilioni 34 zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza sekta ya uvuvi na kilimo cha mwani.
“Katika program ya Sekta ya Maziwa TADB imeweza kupata Shilingi bilioni 16 kutoka taasisi za Bill and Melinda Foundation kwa ajili ya utekelezai wa mradi wa shiriki wa wasindikaji na wazalishaji Maziwa ambapo kupitia program hiyo benki imeweza kutoa mafunzo kwa wafugaji 33,126.
“Imeanzisha vikundi vya wafugaji wanaozalisha maziwa 717 na kusaidia uanzishaji wa vituo vya unywaji wa maziwa 17 ambavyo vina uwezo wa kupokea zaidi ya lita 29,000 kwa wakati mmoja mradi huu unatekelezwa Tanzania Bara na Visiwani (Zanzibar),” amesema Nyabundege
GAWIO LA SERIKALI
Kwa miaka mitatu mfululizo, TADB imetoa gawio kwa Serikali, ambapo katika mwaka 2020 gawio lilikuwa Shilingi milioni 500, mwaka 2021 gawio lilikuwa Shilingi milioni 550 na Mwaka 2022 gawio lilikuwa Shilingi milioni 600.
Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Nevelle Meena, amesema kuwa ni vizuri taasisi na mashirika ya umma wakatoa ushirikiano kwa vyombo vya habari ili kuweza kufikia malengo tarajiwa.