*SASA VIONGOZI WAKE KUPIMWA KILA BAADA YA MIAKA MIWILI, WATAKAOSHINDWA ‘OUT’
NA MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
Msajili wa hazina nchini, Nehemia Mchechu, ametangaza uamuzi mgumu kwa viongozi wa mashirika ya umma ambayo yatashindwa kujiendesha kwa mujibu wa sheria.
Amesema katika mkakati wa sasa wa ofisi ya msajili ni kuhakikisha kila kiongozi atayeteuliwa na mamlaka za uteuzi ni katika kuendesha shirika lazima afanyiwe tathmini ndani ya miaka miwili au mitatu na pindi anaposhindwa atapisha watu wengine.
Hatua hiyo inakuja baada ya hivi karibuni, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kumwagiza msajili wa hazina kuyafuta mashika ya umma ambayo yameshindwa kujiendesha na yamekuwa yakiitia hasara Serikali licha ya kupewa fedha za kujiendesha kwa mujibu wa sheria lakini bado wameshindwa kutoa gawio kwa serikali.
Akizungumza leo Julai 13, 2023 Jijini Dar es Salaam na Wahariri wa vyombo vya habari, Mchechu amesema kwa sasa ofisi ya msajili inasimamia mashirika ya umma 301 kutoka 248 ya awali ingawa kwa baada ya muda mfupi yapo baadhi ya mashirika yataunganishwa hasa baada ya kukamilika kwa kazi ya kupitia muundo wake.
“Juzi sote tulimsikia Rais Dk Samia Suluhu Hassan, akiagiza tuvunje mashika ambayo hayafanyi vizuri licha ya kupewa uwezo wa kujiendesha na serikalli. Lakini kutokana na sasa kutokana na muundo tumeweza kuanza mapya na mengine tutayaunganisha.
“Mashirika yote nchini hasa yale ya umma yanapaswa kuwa ‘active’ (imara) wakati wote na kutoa mchango kwa Serikali. Kwani tunajua yapo baadhi ya mashika yanategemea mchango wa serikali ili yaweze kujiendesha wakati yanatakiwa kujiendesha wenyewe baada ya kupewa mtaji.
“Katika siku 100 za kwanza tumeweza kufanikiwa masuala kadhaa katika mashirika yetu. Ukiangalia makampuni binafsi yanafanya vizuri ikiwamo kampuni kama za Bakhressa, tena huyu ni mtu binafsi ambaye anazalisha kwa wingi na kwa faida kubwa. Au Vodacom inafanya vizuri huku TCCL ikishindwa? kwa nini ya kwetu (Serikali) hayafanyi vizuri licha kuwezeshwa kwa kupewa ruzuku na mitaji,” amesema Mchechu
Msajili huyo wa Hazina, asema kuwa inataka kuenseha mashirika kwa mfumo wa Holding Company (Kampuni Hodhi) ikiwamo kuyaangalia kwa jicho cha biashara kwa kila shirika la umma kwani kutofanya hivyo tija itakosekana.
Amesema katika kusimamia mkakati huo kuanza sasa ofisi yake inataka mashirka yote yawe wazi kwa umma kwa kueleza shughuli zake kupitia vyombo vya habari badala ya kusubiri jicho la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pekee.
“Tunataka kuwepo na ushirikiano kati ya mashirika, Wahariri na waandishi hasa yale ambayo yapo kwa Msajili wa Hazina ikiwamo kutoa taarifa zao kwa mashirika yote ili umma uweze kujua kinachoendelea. Leo ni kuwapa nafasi watanzania badala ya kusubiri mapungufu aliyobaini CAG mashirika yaseme yenyewe na umma ujue kwa uwazi na hii ni sehemu ya mabadiliko ambayo tunakwenda nayo kwa sasa.
“Nchi yetu bado inategemea kilimo na kwa serikali tumeipa uwezo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambaye ni muhusika mkubwa katika kusimamia hili na leo tutaanza nayo kama utaratibu wetu, tunajua wahariri na waandishi mna nafasi kubwa katika kutueleza changamoto zetu,” amesema