Na Mwandishi wetu Dar es Salaam
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Taifa, Sophia Edward Mjema amesema Chama cha Mapinduzi kinawajali wafanyabiashara wadogo na ndio maana kupitia serikali ya awamu ya Sita Chini ya Rais wake Dk. Samia Suluhu Hassan inafanya jitihada kubwa ya kukaribisha wawekezaji katika Taifa lengo likiwa ni kutengeneza fursa nyingi za kibiashara kwa watu wake. ameyasema hayo katika ziara maalum kwenye Masoko jijini Dar es salaam tarehe 15 Julai, 2023
Mjema amesema CCM ndio Chama tawala na kina nia ya dhati ya kuwainua wananchi kiuchumi na hakipo tayari kuona wananchi wake wanafanya biashara katika mazingira Magumu.
“Chama cha Mapinduzi kinatambua kuwa biashara hizi ndio zinawapatia fedha za kujiendesha kiuchumi na nawaambieni maboresho haya ya ujenzi wa masoko ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 kuhakikisha serikali inaboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara kwa watu wake”. Alisema Mjema
Lakini pia Ndugu Sophia Mjema amewasihi Wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwenye jitihada anazozifanya za uwekezaji nchini.
“Ndugu zangu Rais wetu anafanya kazi kubwa sana ya kukaribisha wawekezaji nchini ameifungua nchi na mnaona namna miradi mikubwa ya kimkakati inavyoendelea kutekelezwa kwa kasi, tumuunge mkono ili kuyafikia malengo ya kiuchumi katika Taifa letu”
Mjema amewapongeza sana wafanyabiashara katika soko la Kigogo fresh kwa kuendelea kuwa watulivu licha ya changamoto kadhaa walizozianisha katika soko hilo na kuagiaza Mkuu wa Wilaya na Mkurungezi wa Ilala kuzitafutia ufumbuzi kwa haraka ili wananchi wafanye kazi zao kwenye mazingira rafiki na kwa Uhuru.