NA MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
VIJANA wa Vyama vya siasa waomba kuaminiwa na kudhaminiwa na vyama vyao pale wanapowania nafasi mbalimbali za uongozi hasa katika Uchaguzi Mkuu na chaguzi zinazofanyika ndani ya vyama
Hayo ameyasema Afisa Chadema Digital kanda ya Kaskazini, John Lema akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya majadiliano ya vijana yaliyoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) Agosti Mosi, 2023 katika Ukumbi wa Karimjee Jijinj Dar es Salaam, ambapo amesema vijana wengi hawana vipato ambavyo havitoshi hata kujikidhi maisha yao, kwa hiyo kushiriki kwenye siasa wanatumia nguvu kubwa kuzifikia nafasi wanazozihitaji kisiasa.
Amesema vijana wengi wanadumbukia kwenye ‘Uchawa’ kutumikia watu wengine ili waweze kumpa nafasi au fedha za kufanyia kampeni za siasa njia ambayo ni ya manyanyaso.
“Tunachopambania kwa sasa ni vijana wawezeshwe katika mazingira yatakayo wasaidia kujitegemea wao wenyewe pia katika shughuli rasmi kama ajira ili waweze kujenga vijana wenye uwezo kiuchumi kusudi wakiamua kuanza kupambana kwenye masuala ya siasa waweze kushindana,” amesema Lema
Akizungumzia kuhusiana na mitizamo ya jamii kuhusu vijana, Lema amesema jamii inawaona kama watu ambao bado hawajawa tayari kupewa nafasi za uongozi ingawa kunabaadhi ya vijana wamepewa nafasi na wameonesha uwezo mkubwa ingawa kunabaadhi ya vijana bado hawaoneshi ukomavu pale wanapopewa nafasi na hiyo inaonesha vijana wanatakiwa wakae chini ya wazee.
Pia ametoa rai kwa kijana yeyote atakayepewa nafasi aoneshe uwezo, umakini na uaminifu katika nafasi atakayo pewa na kwenda kuitendea kazi inavyopaswa ili waweze kuwajengea wengine uaminifu pale wanapogombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Ameongeza kuwa destuli na taratibu katika maeneo mengi ambapo vijana ni ngumu kuwaongoza wazee, amesema hizo ni dhana potofu, wawaache vijana waongoze ili wajue ni wapi wanakosea.
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Umoja wa Vijana UVCCM, Mkoa wa wa Dar es Salaam, Ruth Gwajima amesema kuwa ushiriki wa Vijana katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ni mkubwa kwani wamegawanywa katika kakundi tofauti tofauti kama Umoja wa Vijana (UVCCM), Umoja wa Wanawake pamoja na Wazazi.
Amesema kwa kutenganishwa kwa makundi tofauti ni ishara tosha ya vijana kupewa nafasi ili waweze kuwajengea uwezo vijana pamoja na wanawake peke yao kwaajili ya kuwania nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali kichama na Serikali.
“Kwenye CCM kuna tawi, kata, wilaya mkoa na Taifa na vijana wanaruhisiwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi ya tawi mpaka taifa, kijana wa Chama Cha Mapinduzi anaweza kugombea nafasi katika baraza la wanawake na anaweza kugombea kwa Wazazi na CCM,” amesema Ruth
Amesema mara nyingi ushiriki wa vijana ndani ya chama ni kupitia vikao maana vikao vingi vya ndani ya chama na nje ya chama vinawawakilishi wa vijana hivyo basi inasaidia kubeba ajenda za vijana kwa kutoa mapendekezo ndani ya vikao, kwenye mabaraza kuazia ngazi ya tawi na kamati za utekelezaji baada ya hapo mapendekezo yao hufikishwa kwenye vikao vya juu.
Akitolea mfano amesema kuwa mapendekezo ya vijana yanawasilishwa na Mwenyekiti UVCCM kwa kukaa na viongozi wa ngazi ya wilaya ambapo hukaa na viongozi wa serikali pamoja na viongozi wa chama.
Kwa Upande wa Mweka Hazina Ngome ya Vijana Jimbo la Mbagala ACT Wazalendo, Zilfa Kazembwe amesema kuwa changamoto wanazokutana nazo vijana katika kuwania nafasi za uongozi katika chama na Serikali ni uoga wa vijana lakini katika chama wanapata taarifa zote za kuchukua fomu za kuwania nafasi yeyote wanayoitaka.
Amesema changamoto ya kutokuwa na rasilimali fedha ambapo huwawia vigumu kufanya kampeni kwani kunakuwa na mahitaji ya fedha wakati huo hasa katika kuchapisha nakara za matangazo ya uchaguzi, usafiri pamoja na chakula kwa wasaidia kampeni.
“Vijana wengi fedha hatuna, licha ya kuwa na kamati lakini kunamahitaji madogo madogo yanahitaji fedha rasilimali fedha japokuwa tunawatu,”amesema Zilfa
Kwa Upande wa Afisa Program kutoka TCD, Lucy Augustino amesema tayari vijana zaidi ya 300 wameshajadiliana kuhusiana na sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya siasa na mzunguko wa Uchaguzi.
Amesema kuwa majadiliano hayo ni kwa lengo la kuona vijana wanashiriki katika mzunguko wa chaguzi kwani kunashughuli nyingi zinafanyika kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Amesema kunamaboresho mbalimbali yanafanyika katika sheria za Uchaguzi na vyama vya siasa.
“Kwahiyo tunaangalia namna vijana watakavyoshiriki katika hatua zote za uchaguzi lakini hata katika maboresho ya sheria mbalimbali na kuboresha chaguzi zinazofuata. Vijana wanajadiliana na kutupa uzoefu kwa namna gani wanashiriki na kwa namna gani wanaweza kuongeza ushiriki,” amesema Lucy
Akizungumzia kuhusiana na majadiliano hayo, Afisa Program kutoka TCD, Likele Shungu amesema kuwa wanawaandaa Vijana wa Vyama vya siasa ili waweze kushiriki kikamillifu kwenye michakato ya kufanya marekebisho ya sheria za uchaguzi na Vyama vya siasa.
“Hauwezi kufanya marekebisho ya kitu kama hukielewi, kwahiyo tunashirikishana uzoefu katika mambo yanayotokea kwenye shughuli zao za kisiasa, uzoefu walioupata katika Uchaguzi wa miaka ya nyuma pamoja na changamoo ambazo wamewahi kukumbana nazo,” amesema Likele
Amesema lazima vijana waelewe sheria inasema nini ndio waweze kufanya marekebisho katika kipindi cha marekebisho tunachokitarajia.
Vyama vilivyoshiriki program hiyo katika mikoa tisa ni pamoja na CCM, CHADEMA, ACT-WAZALENDO, NCCR – Mageuzi, Chama cha Ukombozi wa Umma na CUF.